Mshikamano na wananchi wa Sardegna waliokumbwa na maafa!
Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za maafa yaliyojitokeza
Kisiwani Sardegna kutokana na mvua kubwa iliyonyeesha ikiambatana na upepo mkali na
hivyo kusababisha watu zaidi ya 16 kupoteza maisha sanjari na uharibifu mkubwa wa
mali. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuungana naye kwa
sala kwa ajili ya waathirika na hasa zaidi watoto wanaoendelea kuteseka kutokana na
janga hili.
Katika ujumbe uliondikwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Pietro
Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wote walioguswa
na janga hili uwepo wake wa karibu hasa kwa njia ya sala. Anawaalika watu wenye mapenzi
mema kuonesha moyo wa mshikamano kwa waathirika wa mafuriko haya ambayo yamesababisha
uharibifu mkubwa wa miundo mbinu.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umetumwa
kwa Askofu Arrigo Meglio, Rais wa Baraza la Maaskofu Sarda, Kusini mwa Italia.