IMBISA inapania kuwa ni kielelezo cha mshikamano na umoja wa Kanisa kusini mwa Afrika!
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA katika mkutano
wake wa kumi, uliohitimishwa hivi karibuni, limekazia umuhimu wa kujenga na kuimarisha
mshikamano wa dhati miongoni mwa Maaskofu na Waamini ili kushuhudia Ukatoliki wao
katika matendo.
Pamoja na mambo mengine, Maaskofu wa IMBISA wamejadili kuhusu
maswali dodoso yaliyotumwa kwao kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi
maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayoadhimishwa mwezi Oktoba 2014 mjini
Vatican.Maaskofu wamejadili kwa kina na mapana kuhusu changamoto, fursa na matatizo
yanayozikabili familia kwenye Nchi za IMBISA na kuamua kwamba, kila Baraza la Maaskofu
lianzishe Idara ya Familia itakayoundwa na Waamini walei pamoja na Mapadre kama sehemu
ya mchakato wa kuendeleza tunu msingi za maisha ya kifamilia Barani Afrika.
Maaskofu
wamekazia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa na kuwataka waamini kuacha mtindo wa ndoa
za majaribio ambazo zinazodhohofisha kwa kiasi kikubwa heshima, heshima na uwajibikaji
wa daima miongoni mwa watu wa ndoa. Waamini watambue maana ya Sakramenti ya ndoa katika
maisha yao ya kiroho na kijamii, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa Familia kama
Kanisa dogo la nyumbani, linalosali na kuhudumiana kwa upendo na ukarimu. Maaskofu
wamekubaliana kimsingi kuanzisha vyama vya kitume vitakavyowasaidia wanandoa wapya
kushauriana katika safari ya maisha yao ya pamoja.
Changamoto inayojitokeza
kwa familia nyingi Kusini mwa Afrika ni ongezeko la familia tenge, zinazohudumiwa
na mzazi wa upande mmoja; familia nyingi kwa sasa zinahudumiwa na wazee wenye umri
mkubwa na kwamba, kuna wasichana wengi wanapata watoto kabla ya kufunga ndoa; hili
ni kundi linalokabiliwa na hali ngumu ya maisha. Kuna ongezeko la watoto yatima na
wale wanaoishi katika mazingira hatarishi kutokana na kuachwa na wazazi wao kwa ugonjwa
wa Ukwimi. Tatizo hili linakwenda sanjari na ongezeko la wajane.
Maaskofu wa
IMBISA wanasema mambo yote haya yanachangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa misingi
thabiti ya maisha ya ndoa na familia Kusini mwa Afrika. Mwaka 2014 ni Mwaka wa Familia
kwa Jumuiya ya Kimataifa ni changamoto wanasema Maaskofu kutumia fursa hii kuimarisha
tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Maaskofu wanasema, IMBISA linapaswa
kuwa ni jukwaa la majadiliano miongoni mwa Maaskofu na mahali pa kutajirishana kiroho,
huku wakipania kusaidiana na kutaabikiana, licha ya tofauti za lugha zinazoweza kuonekana
wakati mwingine kuwa kama kikwazo. Wanasema, wataendelea kusimama kidete kulinda na
kutetea: mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu; utawala bora kwa nchi za SADC.
IMBISA inapaswa kujenga na kuimarisha jukwaa la majadiliano ya kidini na Wakristo
wa madhehebu mengine.
Maaskofu wa IMBISA wameonesha wasi wasi wao kutokana
na kuzuka kwa vita nchini Msumbiji, hali ambayo inaweza kukwamisha juhudi za kujenga
na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Mwishoni, Askofu
Frank Nubuasah kutoka Botswana amechaguliwa tena kuwa Rais wa IMBISA; Makamu wake
ni Askofu Lucio Andrice Mandula kutoka Msumbiji na Askofu mkuu Robert Ndlovu kutoka
Zimbabwe amechaguliwa kuwa Katibu mkuu wa IMBISA.