Viongozi wakuu kutoka Makanisa ya Mashariki na Vatican wanakutana!
Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, kuanzia tarehe 19 hadi tarehe
22 Novemba 2013 linafanya mkutano wake wa Mwaka, unaohudhuriwa na viongozi waandamizi
kutoka Makanisa ya Mashariki pamoja na Vatican.
Wajumbe wanaendelea kuchambua
mafundisho ya Kanisa tangu Karne ya Kumi na nne hadi kwenye Maadhimisho ya Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican na mchango wa Makanisa ya Mashariki katika ustawi na maendeleo
ya Kanisa la Kiulimwengu.
Makanisa ya Mashariki ni kielelezo cha umoja katika
tofauti, kama changamoto ya kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji mpya pamoja na kushirikiana
imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Sheria za Makanisa ya Mashariki zilizochapishwa
kunako mwaka 1990 ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yanayokwenda
sanjari na mabadiliko katika Liturujia kwa Makanisa haya na mwaliko wa kuendeleza
majadiliano ya kiekumene, ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo.
Makanisa
ya Mashariki yanahimizwa kuendeleza Mapokeo ya Kimonaki kama sehemu ya mchango wake
maalum kwa ajili ya ukuaji wa maisha ya kiroho na Kisakramenti, hasa kwa waamini kutoka
kwenye Makanisa ya Mashariki wanaoishi ugenini.
Wajumbe watapata nafasi ya
kuweza kupembua kazi mbali mbali zinazotekelezwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya
Makanisa ya Mashariki na ruzuku inayotolewa kwa Makanisa haya.