2013-11-19 09:13:10

Mwaka wa Imani: Vatican kumekucha! Yaani we acha tu!


Askofu mkuu Rino Fisichella Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yamesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza na kuimarisha moyo wa ibada na sala, waamini wamepata fursa ya kupitia tena nyaraka za Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki; wameshiriki kwa ari na moyo mkuu Ibada na Maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa.

Waamini wamejitahidi kushuhudia imani katika matendo ya huruma na kwamba, ujumbe wa Injili umewafikia watu wengi zaidi. Waamini wamekumbushwa kwa mara nyingine tena kwamba, imani yao inapata chimbuko kutoka kwa Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, tumaini na hija ya maisha mapya!

Kilele cha matukio ya kufunga Mwaka wa Imani ni kuanzia tarehe 21 Novemba 2013, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, sanjari na siku ya kuwaombea Wamonaki, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwatembelea na kusali pamoja na Wamonaki wa Camaldoli walioko mjini Roma.

Ni Watawa wanaotolea maisha yao kwa ajili ya sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kuwahudumia maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii. Ni changamoto kwa waamini kugundua umuhimu wa Neno la Mungu na ushuhuda wa imani tendaji katika matendo ya huruma. Waamini waendeleze ari na mwamko wa kuitafakari sura ya Kristo mteswa kati ya maskini, Neno la Mungu na Sala.

Mwaka wa Imani ulianza kwa Mama Kanisa kuwatangaza: mashahidi na waungama dini pamoja na waalimu wa Kanisa, mwaliko kwa Waamini kujenga na kuimarisha Jumuiya zao, ili ziweze kuwa kweli ni shule ya sala na utakatifu wa maisha; mahali pa kukutana na kuzungumza na Yesu. Mara baada ya Masifu ya Jioni, Baba Mtakatifu atazungumza kwa faragha na Wamonaki hawa na baadaye atakabidhiwa barua za maisha ya kiroho kutoka kwa Sr. Nazarena Crotta, ambaye kunako tarehe 21 Novemba 1945 alijiunga na Wamonaki hawa. Kwa miaka yote ya maisha yake, alikula mkate na maji; alama ya toba, unyenyekevu na utakatifu wa maisha.

Askofu mkuu Fisichella anasema kwamba, tukio kuu katika kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni hapo Jumamosi tarehe 23 Novemba 2013 majira ya jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko atakapokutana na Wakatekumeni walioanza hija ya maisha yao ya Kikristo na kwa sasa wanataka "kuvuka mlango wa Imani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo". Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya kuwapokea Wakatekumeni hawa kama inavyofanyika kwa kuulizwa maswali na baadaye atawaweka Ishara ya Msalaba kwenye paji la uso.

Zaidi ya wakatekumeni 500 wakisindikizwa na Makatekista wao, kutoka katika nchi 47 wanatarajiwa kushiriki, kama kielelezo cha Kanisa la Kiulimwengu. Waamini wanakumbushwa kwamba, wanapokutana na Yesu Msulubiwa maisha yao hayana budi kubadilika na kuanza mchakato wa utakatifu wa maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.