Maisha ya Kikristo yanarutubishwa kwa Sakramenti, Neno la Mungu na matendo ya huruma!
Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa, Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi, Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha umuhimu wa waamini
kuifahamu kwa kina Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa Imani, Sakramenti
za Kanisa, Maisha Adili na Sala inayomwilishwa katika matendo.
Imani thabiti
ni chachu inayomwezesha mwamini kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa
imani yake kwa Kristo na Kanisa lake. Maisha ya Mkristo yanapata mwanzo wake kwa njia
ya Sakramenti ya Ubatizo, mlango wa imani unaomwezesha mwamini kupata Sakramenti nyingine
za Kanisa. Maisha ya mwamini kiroho hayana budi kurutubishwa kwa Sakramenti, Neno
la Mungu na matendo ya huruma.