2013-11-18 08:36:32

Yaliyojiri katika kufunga Mwaka wa Imani, Jimbo kuu la Dar es Salaam


Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho. Ni mlango unomwezesha mwamini kupata Sakramenti nyingine zinazotolewa na Mama Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanafanywa huru toka katika dhambi na wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu na hivyo kuwa ni watoto wa Mungu, viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa na wanaingizwa na kufanywa kuwa washiriki wa maisha na utume wa Kanisa. Ubatizo ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji na Neno.

Maisha ya Kisakramenti yamepewa umuhimu wa pekee katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani katika Majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Katika kuufunga rasmi Mwaka wa Imani, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, amewataka waamini kusimama imara katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, hata pale wanapokabiliana na magumu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha yao.

Kardinali Pengo katika kufunga Mwaka wa Imani, ametoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto zaidi ya mia moja waliotoka katika Parokia 79 zinazounda Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kila Parokia ilikuwa na wajibu wa kuwapeleka watoto wawili ambao wangekuwa ni kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na kuendelezwa kwa kasi na ari kubwa zaidi na Papa Francisko kwa njia ya ushuhuda wa utume na maisha yake.

Mwaka wa Imani, ilikuwa nifursa ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuanza mchakato wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa njia ya ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kardinali Pengo anasema, kuna baadhi ya waamini ambao bado wanashindwa kuimwilisha imani yao katika matendo, kwa kukiishi kile wanachoungama katika Kanuni ya Imani, kile wanachoadhimisha katika Liturujia na Sakramenti za Kanisa; kile wanachojitahidi kukiishi kwa kuongozwa na Amri kumi za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha adili na hatimaye, kile wanachokisali na kukimwilisha katika matendo ya huruma.

Kardinali Pengo amewataka waamini Jimbo kuu la Dar es Salaam, kuishi kikamilifu wito na dhamana yao kama Wafuasi wa Kristo kwa kutenda yale yanayo mpendeza Mungu na mwanadamu. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Jimbo kuu la Dar Es Salaam, limezindua Kitabu cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki, mwaliko wa kuendeleza kuyakiri, adhimisha, ishi na kusali yale yote waliojipatia wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Kardinali Pengo anasema, kufungwa kwa Mwaka wa Imani Jimbo kuu la Dar es Salaam ni mwanzo wa mchakato wa kuimwilisha Imani katika matendo, kwani kila Mwaka ni Mwaka wa Imani, kwa kuendeleza mema na mazuri waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu hata pasipo na mastahili yao. Mwaka wa Imani umekuwa na mafanikio makubwa kwa waamini Jimbo kuu la Dar es Salaam.







All the contents on this site are copyrighted ©.