2013-11-18 12:14:55

Utamaduni wa utandawazi unaotaka kusawazisha yote ni chanzo cha majanga na maafa makubwa katika maisha ya mwanadamu!


Mwenyezi Mungu anapenda kuwakomboa waja wake ili wasimezwe na malimwengu, kwa kujikita zaidi na zaidi katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili, wakijishikamanisha na imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kuna haja kwa waamini kuwa makini zaidi na utandawazi unaotaka kusawazisha mambo yote kuwa ni sawa. Kuna haja ya kujenga kuimarisha mshikamano wa upendo na kidugu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuwa waaminifu kwa mpango wa Mungu na maendeleo ya binadamu.

Hii ni sehemu ya Mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 18 Novemba 2013 kama sehemu ya kumbu kumbu ya kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika utekelezaji wa ahadi zake, hata pale Taifa la Israeli lilipokengeuka na kuanza kumwasi Mwenyezi Mungu aliyefunga nao Agano la Kale.

Utamaduni wa utandawazi unaotaka kusawazisha mambo yote hata yale yanayogusa maisha ya watu kiroho ni hatari, kama ilivyojionesha kwa Waisraeli kwa kumwasi Mungu na Amri zake; wakakengeuka kwa kupotoshwa kutokana na kuiga Mataifa jirani. Madhara yake ni maafa na majanga yanayoendelea kumong'onyoa maadili na utu wema, kiasi hata cha kukumbatia utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu anaendelea kuwakumbusha waamini kwamba, Mwenyezi Mungu daima ataendelea kuwa mwaminifu; yuko tayari kusamehe na kuwaokoa wale wanaomkimbilia kwa moyo radhi na toba. Atawalinda na kuwavusha katika hatari kama alivyofanya kwa Waisraeli, kwani mikononi mwa Mwenyezi Mungu, mwanadamu atapata amani na usalama wa maisha yake.







All the contents on this site are copyrighted ©.