2013-11-18 08:14:01

Tanzania yakabidhiwa taarifa kuhusu ugonjwa wa mnyauko wa minazi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake imedhamiria kukabiliana na maradhi ya mazao likiwamo zao la mnazi ambalo linakabiliwa na tatizo la mnyauko. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu kwa Serikali kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo la minazi kwa sababu watu wengi katika baadhi ya maeneo ambayo uchumi wake unategemea zao la mnazi wanakabiliwa na hatari ya kweli kweli ya kuathirika kwa maisha yao.

Rais Kikwete ametoa uhakikisho huo Jumamosi, Novemba 16, 2013, wakati alipokutana na Waziri wa Maendeleo ya Minazi na Maendeleo ya Shamba la Janatha wa Sri Lanka, Mheshimiwa Jagath Pushpakumara na ujumbe wake mjini Colombo. Waziri huyo aliandamana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti ya Minazi ya Sri Lanka.

Rais Kikwete yuko nchini Sri Lanka kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaomalizika leo, Jumapili, Novemba 17, 2013. Mkutano huo wa siku tatu, ulianza Ijumaa, Novemba 15, 2013. Mheshimiwa Pushpakumara na ujumbe wake walikuwa wanamwelezea na kumkabidhi Rais Kikwete Ripoti ya Magonjwa ya Minazi iliyoandaliwa na wataalam wa minazi wa Sri Lanka ambao walitembelea Tanzania Julai mwaka huu.

Wataalam hao walitembea Tanzania na kufanya utafiti kuhusu ugonjwa unaolikabili zao la minazi kufuatia ahadi ya Rais Mahinda Rajapaksa aliyoitoa kwa Rais Kikwete wakati alipofanya ziara rasmi ya Tanzania Juni 27, 2013, na baadaye kushiriki katika Mkutano wa Smart Partnership Juni mwaka huu.

Rais Rajapaksa alitoa ahadi hiyo baada ya kuelezwa na Rais Kikwete kuhusu zao la kukauka kwa minazi nchini. Minazi ni zao muhimu sana katika uchumi wa Sri Lanka na ni zao tegemeo kwa wananchi wa Taifa-Kisiwa hilo kilichoko kusini mashariki mwa India katika Bahari ya Hindi. Wataalamu waliofuatana na Waziri huyo wamemwambia Rais Kikwete kuwa ugonjwa unaolikabili zao hilo la minazi ambao pia unashambulia minazi katika eneo la Caribbean hauna tiba kwa sababu mpaka sasa hakuna taasisi yoyote ya utafiti imegundua dawa hiyo.

Wataalam hao ambao walikaa Tanzania kwa wiki moja, zikiwamo siku mbili katika Zanzibar, wanasema kuwa zao hilo la mnazi, kama ilivyo katika nchi nyingine zinazolima zao hilo, lina uwezo mkubwa wa kusaidia uchumi kupitia viwanda vidogo vidogo. Wakati wakiwa Tanzania, wataalam hao wa Sri Lanka walifanya uchunguzi na utafiti kwa karibu na wataalam wa Taasisi ya Utafiti ya Kilimo ya Mikocheni (MARI).

Rais Kikwete azungumza kwa ajili ya viongozi wenzake Sri Lanka

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa maoni ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 yatakuwa mchango mkubwa kuhusu nini kifanyike baada ya kumalizika kwa kipindi cha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG).

Aidha, Rais Kikwete ameipongeza nchi ya Sri Lanka kwa kuandaa vizuri na kwa mpangilio mzuri Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliomalizika mchana wa leo, Jumapili, Novemba 17, 2013.

Rais Kikwete ameyasema hayo na kutoa pongezi hizo Jumamosi, Novemba 16, 2013, wakati alipotoa Salamu za Shukrani kwa niaba ya viongozi wote waliohudhuria Mkutano huo kwenye Chakula cha Usiku rasmi kilichoandaliwa na Rais wa Sri Lanka, Mheshimiwa Mahinda Rajapaksa kwenye Ikulu ya Temple Trees ya nchi hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Rais Kikwete amesema: “Mada ya mwaka huu ya mkutano wetu wa CHOGM ya Maendeleo ya Pamoja kupitia Ukuaji wa Pamoja imekuja kwa wakati unaofaa. Kwa taasisi kama ya kwetu ambayo inawakilisha watu bilioni mbili kujadili suala hilo hasa kwa kutilia maanani mjadala unaoendelea kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 ni jambo la busara sana.”

Mkutano wa CHOGM ambao ulianza Ijumaa, Novemba 15, 2013, umemalizika Jumapili tarehe 17 Novemba 2013 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kumbukumbu ya Bandaranaike mjini Colombo, Sri Lanka.

Akizungumzia mkutano huo, Rais Kikwete amesema: “Tunakupongeza Mheshimiwa Rais kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huo. Tunajua siyo kazi rahisi kuandaa Mkutano wa ukubwa huu. Lakini kwa uongozi wako wa busara na uongozi wako, kwa kusaidiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, kila kitu kimekwenda vizuri.” Ameongeza Rais Kikwete: “Kwa niaba ya viongozi wenzangu waliokusanyika hapa jioni ya leo, napenda kukutakia wewe, Mheshimiwa Rais, kila la heri katika uendeshaji wa taasisi yetu hii.”








All the contents on this site are copyrighted ©.