Onjeshaneni tone la furaha, matumaini na machungu ya maisha kwa kulinda na kutetea
utu na heshima ya binadamu!
Jumuiya ya Kimataifa inaanza kugundua tena umuhimu wa kujenga na kudumisha mshikamano
wa dhati miongoni wa Jamii mbali mbali kama njia ya kupambana na majanga ya maisha,
ili kwa pamoja kama Jumuiya waweze kuonjeshana tena tone la furaha, matumaini na machungu
ili kwa pamoja waweze kukumbatia zawadi ya maisha! Binadamu anapaswa kupewa kipaumbele
cha kwanza na viongozi wa kisiasa na kidini, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea
utu na heshima yake na kamwe asiwe ni kichokoo cha udadisi wa tafiti za kisayansi.
Majadiliano
ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali yanawachangamotisha wadau kuhakikisha
kwamba, wanaheshimu dini na mafundisho tanzu ya kila dini; kutobeza dini za watu wengine
pamoja na kuthamini tofauti mbali mbali zinazojitokeza miongoni mwa Jamii, kwani huu
ni utajiri mkubwa na wala si tishio kwa amani, usalama na ustawi wa Jamii husika.
Huu ni mchango wa Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la
Majadiliano ya kidini wakati alipokuwa anachangia kwenye Semina iliyoandaliwa na Kituo
cha Majadiliano ya Kidini na Kitamaduni cha Mfalme Abdullah Bin Aziz, kwa kifupi KAICIID
huko Vienna, Austria, tarehe 18 Novemba 2013 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Sura ya
mwingine".
Anasema, majadiliano ya kidini yanaweza kusaidia mchakato wa kumpatia
Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha ya watu; kujenga na kudumisha mshikamano
wa kidugu pamoja na kuwa nari ya kutenda kwa ujasiri. Majadiliano ya kidini yasaidie
kusafisha dhamiri na kuwa tayari kupokea mawazo mapya kutoka kwa wengine sanjari na
kukubali changamoto zinazotolewa katika masuala ya imani, kwa ajili ya mafao ya wengi.
Waamini wajifunze kuheshimiana na kuthaminiana kwani wameumbwa kwa sura na
mfano wa Mungu.