2013-11-18 11:45:04

Mwanadamu amekuwa ni adui mkubwa wa mazingira!


Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, CISDE kwa kushirikiana na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, yameandaa mkutano wa siku mbili, uliofunguliwa tarehe 18 Novemba 2013 na unatarajiwa kufungwa hapo tarehe 19 Novemba 2013, ili kuweza kupembua kwa kina mchango wa Kanisa katika kukuza na kudumisha haki ya mazingira bora.

Askofu mkuu Celestino Migliore, Balozi wa Vatican nchini Poland anasema, kwamba, kuanzia mwaka 1992 Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikijadili mbinu mkakati wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi bila mafanikio makubwa. Itifaki ya Mkataba wa Kyoto wa Mwaka 1997 ukazilazimisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, lakini bado kuna kinzani zinazooneshwa na Nchi zilizoendelea na Nchi zinazoendelea duniani kwa kukosa utashi wa kisiasa katika utekelezaji wa makubaliano yanayofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi unaofanyika mjini Varsavia unaweza kusaidia kuweka mikakati bora zaidi ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kanisa linashiriki kikamilifu katika mikutano hii ili kuweza kuchangia kwa kina na mapana umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa kama njia ya kupambana na majanga yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kwa pamoja Jumuiya ya Kimataifa iweze kufikia muafaka kwa ajili ya mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho! Vatican inashiriki kwa kuhimiza usawa na utofauti katika utekelezaji wa mikakati ya udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi.

Usawa huu unajikita katika kipimo cha pato ghafi la taifa; uzalishaji wa hewa ya ukaa unaofanywa na nchi husika katika uchafuzi wa mazingira, ili kwamba, wale wanaochafua zaidi walipie zaidi. Hii inaonesha kwamba, ufundi na sayansi vizipozingatiwa barabara, Jumuiya ya Kimataifa haitakuwa na uwezo wa kukabiliana na majanga yanayoendelea kujitokeza katika uso wa dunia. Mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kusababisha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, jambo linalohitaji mshikamano wa kimataifa ili kufikia suluhu ya kudumu. Jamii inapaswa kujenga dhamiri nyofu kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utunzaji bora wa mazingira.

Huu ndio mchango ambao umetolewa na Mama Kanisa kwa karne nyingi katika maisha na utume wake kwa kutambua kwamba, mazingira ni sehemu ya kazi ya uumbaji na zawadi ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu kuilinda na kuitunza kwa ajili ya kizazi hiki na kile kijacho. Takwimu zinaonesha kwamba, binadamu anaendelea kuwa adui mkubwa wa mazingira kwa matumizi yasiyokuwa na tija wala kujali mafao ya wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.