Jengeni Maktaba ili ziweze kuwa ni vituo vya rejea kwa wasomi!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema kila Halmashauri nchini Tanzania inapaswa
kuweka kwenye mpango wake wa maendeleo kifungu cha ujenzi wa maktaba ya wilaya ili
watu waweze kusoma na kujiendeleza kwa urahisi. Ametoa kauli hiyo Novemba 16, 2013)
wakati akiwahutubia washiriki wa mahafali ya 19 ya Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi wa
Nyaraka cha Bagamoyo yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho nje kidogo ya mji
wa Bagamoyo.
Jumla ya wahitimu 749 walitunukiwa vyeti kati yao 244 vikiwa
ni vya stashahada na 505 ni vya astahada katika fani za ukutubi na utunzaji nyaraka.
Alisema
ukutubi ni mojawapo ya fani kongwe hapa duniani japo haiongelewi sana hapa nchini.
“Hili ni eneo linalomgusa kila mmoja wetu, kuanzia mtu wa kawaida awe mkulima, mvuvi,
seremala, mjasiriamali ama yeyote ambaye anahitaji taarifa mbalimbali zimsaidie katika
maendeleo yake. Hali kadhalika, mwanafunzi, msomi na mwanataaluma yeyote hawezi kufikia
upeo wa masomi na taaluma yake kama hakusoma vitabu na machapisho yaliyoko katika
maktaba ambavyo vinatunzwa mkutubi.
Alisema kati ya wilaya 133 zilizopo hapa
nchini, ni wilaya 19 tu ambazo zimejenga maktaba katika ngazi ya wilaya. “Hii ni sawa
na asilimia 14.2 tu ya wilaya zote. Upungufu huu unasababishwa na tatizo la watu kutotambua
umuhimu wa kuwa na maktaba na katika hili lawama ni lazima wabebeshwe Wakurugenzi
wa Halmashauri,” alisema. Waziri Mkuu alisema katika ngazi ya mikoa hali si mbaya
kwani mikoa 22 kati ya 25 ya Tanzania Bara ina maktaba za mkoa.
“Tunazo Halmashauri
167 lakini ni Halmashauri 19 tu ambazo zina maktaba... nitoe wito kwa wilaya zote
ambazo hazina maktaba zione umuhimu wa kuwa na maktaba zake. Tukifanikiwa kuwa na
maktaba katika kila mkoa na kila wilaya itatuwia rahisi kuisogeza huduma hiyo katika
ngazi ya kata ili iwe karibu zaidi na wananchi,” alisema.
Akisisitiza umuhimu
wa fani hiyo Waziri Mkuu alisema mahitaji ya wakutubi hapa nchini ni makubwa kwani
hapa nchini kuna shule za msingi zaidi ya 16,300 na shule za sekondari zaidi ya 4,500
za Serikali na za binafsi.
“Tunawahitaji zaidi hawa wakutubi katika shule zetu
kwani wakiwepo kwenye shule zetu watakuwa karibu na wanafunzi na wataweza kuwasaidia
wanafunzi kupanua uelewa wao,” alisisitiza. Aliahidi kufuatilia maombi ya bajeti ya
maendeleo ya chuo ili kukisaidia chuo hicho kiwe bora zaidi.
Mapema akitoa
taarifa ya chuo hicho, Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Zuberi Khatibu alisema chuo hicho kinakabiliwa
na changamoto ya uhaba wa madarasa licha ya kuwa udahili umekuwa ukiongezeka mwaka
hadi mwaka.
“Mwaka 2007/2008 chuo kilidahili wanafunzi 100 lakini katika mwaka
2012/2013 tulidahili wanafunzi 708 na mwaka huu wa masomo (2013/2014) tumedahili wanafunzi
821,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Dk. Alli Mcharazo,
alisema kabla chuo hicho hakijaanzishwa hapa nchini, wanafunzi waliokuwa wakitaka
kusomea masomo ya ukutubi na uhifadhi nyaraka walilazimika kwenda Makerere, Uganda.
Alisema
mbali ya uwepo wa chuo hicho, changamoto kubwa inayowakabili ni ufinyu wa bajeti,
uhaba wa miundombinu hasa upungufu wa mabweni na madarasa kiasi kwamba wanalazimika
kuwa na shift mbili za masomo (asubuhi na jioni) hali ambayo inaathiri utoaji wa elimu
chuoni hapo.
Katika risala yao, wanafunzi wanaohitimu waliomba wapatiwe ajira
za moja kwa moja kama ilivyo kwa walimu au askari, pia waliomba maktaba ya chuo hicho
ipanuliwe kwa sababu ni ndogo na ikiwezekana chuo kiongezewe kompyuta kwa sababu zilizopo
hazitoshi wanafunzi wote kufanya mazoezi kwa vitendo.