Vijana mnapaswa kuwa ni Wamissionari wa Injili, kila siku na kila mahali!
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii,
kwa namna ya pekee, leo anapenda kuwaalika vijana kuwa ni Wamissionari wa Injili,
kila siku na kila sehemu.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amechagua
tema zitakazoongoza Maadhimisho ya Siku ya za Vijana Duniani kwa kipindi cha Miaka
mitatu, kama sehemu ya maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani itakayofanyika mjini Cracovia,
Poland, kunako Mwaka 2016. Mada zilizochaguliwa na Baba Mtakatifu ni kutoka katika
Heri za Mlimani, ambazo kimsingi ni Muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo.
Siku
ya 29 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2014 itaongozwa na kauli mbiu: "Heri maskini wa
roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Mt. 5:3.
Siku ya 30 ya Vijana Duniani
kwa Mwaka 2015 itaongozwa na kauli mbiu "Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona
Mungu.
Siku ya 31 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 itakayofanyika Jimbo kuu
la Cracovia, Poland, itasindikizwa na mada "Heri wenye rehema maana hao watapata rehema."
Mt. 5:7.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na bahari
ya vijana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 mjini Rio
de Janeiro, nchini Brazil, aliwaalika vijana kufanya tafakari ya kina kuhusu heri
za Mlimani ili hatimaye waweze kuzimwilisha katika uhalisia wa maisha yao.
Hii
ni kutokana na ukweli kwamba, Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya
Kristo na ni kanuni na mwongozo wa maisha ya kiroho!.