Jubilee ya Miaka 50 tangu Mashahidi wa Uganda kutangazwa kuwa Watakatifu, Papa Francisko
anaalikwa na Maaskofu wa Uganda!
Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, limetoa mwaliko kwa Baba Mtakatifu Francisko,
kutembelea nchini Uganda, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 tangu
Mashahidi wa Uganda walipotangazwa na Mama Kanisa kuwa ni watakatifu, kielelezo na
mfano wa kuigwa katika imani na maisha adilifu.
Kilele cha Maadhimisho haya
ambayo nchini Uganda yamekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kitakuwa
hapo tarehe 18 Oktoba 2014, wakati ambapo Madhabahu ya Namgongo yatakapofurika kwa
umati wa mahujaji kutoka ndani na nje ya Uganda. Mashahidi wa Uganda walitangazwa
kuwa Watakatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hapo tarehe 18
Oktoba 1964.
Nia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, ilibainishwa na Askofu
mkuu Cyprian Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala alipokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu
Francisko, hapo tarehe 21 Septemba 2013 mjini Vatican. Ikiwa kama Baba Mtakatifu Francisko
ataridhia hija hii ya kichungaji, pengine itakuwa ni hija ya kwanza kwa Baba Mtakatifu
kulitembelea Bara la Afrika tangu alipochaguliwa.
Mwenge maalum wa Maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Mashahidi wa Uganda walipotangazwa kuwa watakatifu unaendelea
kuzunguka katika Parokia 54 zinazounda Jimbo kuu la Kampala, kama kikolezo cha ushuhuda
wa imani tendaji katika kuikiri, adhimisha, mwilisha na kusali imani ambayo ni zawadi
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini inamwajibisha mwamini kuitolea ushuhuda, ili Kristo
aendelee kuwa ni Mwanga wa Mataifa.