2013-11-16 10:56:19

Hija ya kihistoria iliyofanywa na Papa Paulo VI nchi Takatifu


Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki, Papa Paulo VI, kuanzia tarehe 4 hadi 5 Januari 1964 alifanya hija ya kichungaji katika Nchi Takatifu kama njia ya kuimarisha majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali wanaoishi huko Mashariki ya Kati.

Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia, tarehe 15 Novemba 2013 limefanya kumbu kumbu ya tukio hili la kihistoria kwa njia ya Kongamano pamoja na kutembelea yaliyokuwa makazi ya Kardinali Giovanni Battisti Montini, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano, kabla ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, sanjari na Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu alipochaguliwa kuwa Papa.

Kongamano hili limelenga pamoja na mambo mengine kutembea katika nyayo za Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI mintarafu nyayo za Mtakatifu Petro. Waamini wamepata kuangalia tena picha muhimu zilizopigwa wakati Papa Paulo VI akipokuwa anafanya hija ya kichungaji kwenye Nchi Takatifu. Hizi ni picha zilizopigwa kunako mwaka 1964, siku sita kabla ya kuzuka vita huko Israeli.

Picha hizi zinaonesha pia siku ile Papa Paulo VI alipokutana na kuzungumza na Patriaki Atenagoras wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli kama mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kiekuemen baina ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox, mazungumzo ambayo yalipelekea kutiwa sahihi kwa hati maalum baina ya viongozi hawa wawili wa Kanisa.

Kongamano hili la siku moja, limehudhuriwa na viongozi mbali mbali kutoka Nchi Takatifu kama njia ya kuimarisha uhusiano wa kiekumene katika mchakato wa kutafuta umoja kamili miongoni mwa Wafuasi wa Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.