Balozi wa Vatican nchini Tanzania awataka waamini kuendelea kuwa ni chumvi na mwanga
wa mataifa!
Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi
wa Vatican nchini Tanzania wakati wa Ibada ya kufunga Mwaka wa Imani nchini Tanzania,
hapo tarehe 10 Novemba 2013, Parokiani Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro. Ibada
ambayo ilihudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu nchini Tanzania.
Mwadhama Ndugu
zangu Maaskofu Wakuu na Maaskofu Wapendwa Mapadri, watawa, viongozi wa serikali Wapendwa
waamini.
Tunapo adhimisha Misa hii ya kufunga rasmi Mwaka wa Imani kitaifa,
ningependa nianze na maneno ya Kristo anayesema: “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu,
ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani” (Yn 12:46).
Mwanga huu ulikuja
duniani miaka elfu mbili iliyopita. Mwanga huu ndiyo tabia ya Ufalme wa Mungu, ulio
anzishwa na Kristo Mfalme. Alikuja kusimika Ufalme hapa duniani, ufalme ambao si mamlaka
ya dola bali Ufalme wa Imani unao dhihirika katika upendo na heshima.
Sisi
ni sehemu ya ufalme huu. Sisi pia tumepokea mwanga huu, imani hii mioyoni mwetu iliyoletwa
na wamisionari shupavu. Kwa namna ya pekee nawashukuru Mapadri wa Shirika la Roho
Mtakatifu kwa majitoleo na sadaka zao katika kuleta mwanga huu, imani hii ambayo ilianzia
Zanzibar na kuingia Bara kupitia Bagamoyo. Hii ndiyo sababu tunaadhimisha Misa hii
mahali hapa.
Watu waliifurahia imani hii, waliufurahia mwanga huu. Lakini
hapo katikati, imani ikahusishwa na giza. Watu wengi wakaacha kuihusisha imani na
Kristo wakaihusisha na wanadamu, hivi kwamba kiini cha imani kikawa si Kristo tena
bali watu. Huu ukageuka kuwa mwanga binafsi, ulioweza labda kuufurahisha moyo na kumfariji
mtu binafsi lakini si tena mwanga unaoweza kupendekezwa kwa wengine kama mwanga halisi
na ambao watu wanaweza kuushiriki na kuona njia. Unapopotea mwanga huu mkubwa ambao
ni Yesu Kristo, kila kitu kinatatanisha. Inakuwa ni vigumu kupambanua wema na uovu,
au njia inayotuongoza kwenye lengo letu na zile njia zisizo tufikisha popote. Ufalme
wa Mungu uliojengwa duniani umepitia katika hali ya kumfanya Mungu asionekane na watu
kuishi katika “jangwa” la kiroho.
Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia
jinsi ambavyo maisha au dunia bila Mungu jinsi ilivyo. Sasa tunaiona hali hiyo kila
siku katika maisha yetu. Utupu umeongezeka. Kwa watu wengi tatizo kati ya imani na
maisha limeongezeka. Lipo hitaji la lazima sasa kuhakikisha kwamba imani inakuwa tena
mwanga, yaani Yesu Kristo mwenyewe, anayeweza kuangaza kila hali ya maisha ya mwanadamu.
Ndiyo maana Mwaka wa Imani ulianzishwa na Papa Benedikto na kuendelezwa na
Papa Fransisko kwa lengo la kupambana na tatizo la kupotea kwa imani ili kujitahidi
kuirudisha imani mahala pake: yaani imani kwa Kristo na siyo imani kwa ubinafsi wa
mtu. Imani ya kweli inazaliwa katika kukutana na Mungu aliyehai ambaye anatualika
na kuufunua upendo wake, upendo ambao tunaweza kujifunza ili utulinde na utusaidie
kujenga maisha ya watu. Wakigeuzwa na upendo huu, watu wa Ufalme wa Mungu hapa duniani
wanapata muono mpya, macho mapya yanayo wafanya kutambua kuwa imani inabeba ahadi
kubwa ya maisha mema na kwamba dira ya maisha yajayo inafunguka mbele ya kila mmoja.
Mwaka
wa Imani umewafanya kugundua na kuuiona sura ya Kristo. Na mtu anapoiona sura ya Kristo,
basi upendo unaumbwa katika moyo wake na kumgeuza kuwa mtu anaye hamasisha upendo
katika jamii ya leo. Kwa hiyo imani hii mpyainazaa upendo na kwa upendo huu mtu anakuwa
mwanga wa ulimwengu. Kwa nini leo hii kuna chuki sana katika jamii? Kwa sababu hakuna
mwanga na upendo. Kwa kuadhimisha mwaka wa imani mtu anakuwa mwanga unaofuatwa na
wengine kwa kuendeleza kazi za Kristo, kazi za upendo, msamaha, maridhiano na amani.
Kwa ufupi, Mwaka wa Imani umewaalika kuwa mashahidi wa kweli wa Kristo kwa wengine.
Haiwezekani tena baada ya maadhimisho haya ukabaki kuwa mtu uliyejitenga, unaye tumainia
nafsi yako na ubinafsi wako kama msingi wa matendo yako
Watu huishi daima katika
uhusiano. Unatoka kwa wengine, wewe ni wa wengine na maisha yako lazima yatajirishwe
kwa kukutana na wengine. Mioyo yenu itajazwa na imani hii, itajazwa na nafsi ya Kristo
ili kwamba pasiwepo tena nafasi ya chuki, wivu, ubinafsi. Unakuwa mmisionari wa kweli
wa Yesu Kristo, ukidumisha amani, msamaha na maridhiano, ambazo ni sifa za Ufalme
wa Mungu duniani, ufalme ambao dunia inautamani sana leo hii.
Ndiyo,
baada ya mwaka wa imani, mnapewa utume wa kuwa mwanga na chumvi ya ulimwengu. Na katika
kutekeleza utume huu, matatizo yatakuwa mengi kwa sababu mtakutana na mbwa mwitu walio
tayari kuwa rarua wale wanaopeleka ujumbe wa Yesu Kristo. Ndugu zangu, hiyo ndiyo
hali yetu: sisi ni wamisionari waliotumwa kama kondoo kati ya mbwa mwitu ili kutangaza
ujumbe wa upendo, msamaha, maridhiano na amani katika dunia iliyojaa vurugu. Wamisionari
siyo wale tu walioacha familia na nchi zao kwenda kutangaza injili. Sisi sote, kadiri
ya hali zetu za maisha, kwa ubatizo wetu na kwa imani tuliyoipokea ni wamisionari
na ni wajibu wetu kutimiza wito wetu wa kuwa watatkatifu katika maisha na kupanda
duniani injili ya upendo na amani.
Mtu anawezaje kuwa nuru na chumvi ya
dunia? Baada ya maadhimisho haya ya mwaka wa imani, kila mmoja wetu anapaswa kujichunguza
na kutafakari kama yametokea mabadiliko yoyote moyoni mwake; kama amegundua utume
wa maisha yetu wa kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani. Jamii ambamo upendo, kuheshimiana
na haki vinatawala. Mwaka wa imani unadai wale wote walio na wajibu wa kisiasa, kiuchumi
na katika masuala ya jamii kuwa na ujuzi juu ya mafundisho ya jamii ya Kanisa, ambayo
yanaweza kuwapatia misingi ya kutenda kulingana na Injili. Watu hawa wanatakiwa kuwa
mashuhuda wa kikristo na wataamika pale tu watakapo fanya kazi zao kwa uaminifu na
weledi; pale tu watakapokuwa na imani itakayo waongoza kutenda kwa upendo na kuwahudumia
watu wote, hasa masikini.
Imani hii inapaswa kutuwezesha, kwanza kabisa, kuheshimu
mazingira na kutambua sarufi iliyoandikwa kwa mkono wa Mungu kuwa ni mahali pa kuishi
ambapo kila mmoja anapaswa kupalinda na kupatunza. Imani hii itawawezesha watu kutafuta
namna za maendeleo ambazo msingi wake siyo tu matumizi na faida bali yale yaliyo mema
na ya haki katika jamii. Imani hii itatufundisha kuunda mifumo ya uongozi iliyo ya
haki kwa kuunda dhamiri za wale wanaoongoza kutambua kuwa mamlaka hutoka kwa Mungu
na yapo kwa ajili ya kuhudumia manufaa ya wote. Imani hii itatupatia fursa ya kusamehe,
jambo ambalo mara nyingi linahitaji muda, jitihada, uvumilivu na uthabiti. Msamaha
unawezekana pale mtu anapogundua kwamba wema unashika mahali pa kwanza na una nguvu
kupita uovu na kwamba neon la Mungu lina nguvu kuliko mtu anavyoweza kulikataa.
Katika jamii yetu leo, tunahitaji wakatoliki ambao ni mfano wa fadhila zinazo
hubiriwa katika Injili, maisha ya ushuhuda wa upendo, maridhiano na amani. Kama bado
hatuweza kuzalisha wakatoliki wa namna hii au kama tunaona kila wanacho amini hakipatani
na kile wanachoishi, hapo tujue kwamba bado tuna kazi ya kufanya ili kupata watu waadilifu
na wenye imani. Ni wajibu wetu kuwaonesha watu tena uzuri, wema na ukweli wa sura
ya Kristo ambao ndani yake kila mwanadamu anaalikwa kutambua kielelezo cha kweli cha
kufuata. Kwa hiyo hii ndiyo changamoto yetu kubwa baada ya mwaka wa imani: kuwaelekeza
watu wa leo kwa Kristo, kumtambulisha kama kipimo cha kweli cha ukomavu na ukamilifu
wa mwanadamu.
Katika Bara la Afrika, hali halisi inadai uwezo wa kujumuisha
makuzi ya kiakili ya imani na uzoefu wa maisha ya kukutana na Kristo aliye hai na
anayetenda katika jumuiya ya kikanisa. Mapadri na Maaskofu mnapaswa kusisitiza ukweli
kwamba kuwa mkristo si matokeo ya maamuzi ya kimaadili bali kukutana na nafsi ya Kristo.
Waamini wanapaswa kufundishwa kuwa daima umoja ni bora kuliko mafarakano na palipo
na mafarakano ya watu na maslahi, si vema kupuuzia. Ni muhimu kukabiliana na hayo
kwa lengo la kutafuta ufumbuzi na kusonga mbele katika kufikia umoja na maridhiano.
Ni
wajibu wetu kama viongozi kuitunza imani hii ndani ya watu wetu. Imani na upendo vinapodhoofika,
misingi ya ubinadamu nayo inatiwa hatarini. Ndiyo, kama tutaondoa imani kwa Mungu
katika miji yetu, kuaminiana kutatoweka. Watu watabaki wameungana katika hofu na uthabiti
utapotea. Sote tunapaswa kuwa mwanga kwa wale walio bado gizani, wale wasiofahamu
bado hali za wanadamu na matukio. Imani yenu leo itakuwa taa ya kuongoza hatua zenu
katika usiku maisha na katika safari yenu ya upendo, msamaha, maridhiano na amani.
Ninawaalika tuimarishwe kwa maneno ya Kristo: Msiogope, niko pamoja nanyi
mpaka ukamilifu wa dahari. Katika wakati wa shida na majaribu, zawadi hii bora ya
imani leo iwaongoze kwenye matumaini, matumaini yanayoangalia mbele katika ufahamu
kwamba ni katika nafsi ya Yesu Kristo pekee ndimo nafsi zetu na Kanisa letu na jamii
yetu inamoweza kupata misingi imara nay a kudumu. Ni katika muungano wa imani na upendo,
matumaini yanatuongoza katika safari ya kuelekea siku zijazo kwa hakika na kufutilia
mbali kudanganywa na mali za dunia. Msihurusu kuibiwa matumaini haya ambayo yanawatia
ujasiri wa kusonga mbele hata katika hali ngumu.
Mwaka wa Imani ni mwanzo
tu. Tutaendelea na safari ili kutajirisha maisha yetu kwa nafsi ya Yesu Kristo. Huyu
ndiye atakaye tufanya kuwa vyombo vya mabadiliko kwa jamii. Tuombe mwaka huu wa imani
uwe tukio lenye kuzaa matunda kwa kila mmoja wetu kukuza uhusiano wake na Munguna
wengine. Mwaka huu uwaimarishe muweze kujenga utamaduni wa upendo kwa kutoa msamaha,
kusaidia maridhiano na amani.
Ninaomba ili tuweze kusambaza tunu hizi bora
kwa jamii na ulimwengu upate kuwa mahali pazuri kuishi kulingana na mfumo wa Ufalme
wa Mungu uliojengwa na Kristo kwa ajili yetu, ambamo wote tunakuwa kielelzo cha fadhila
za msamaha, maridhiano na amani sasa na hata milele.