Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya nchi!
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa ziara yake ya kikazi kwenye Ikulu ya Italia, Alhamisi,
tarehe 14 Novemba 2013, amemshukuru Rais Giorgio Napolitano kwa kumpatia nafasi ya
kuweza kukutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Ikulu ya Italia pamoja na familia
zao. Amewataka wafanyakazi hao kuonesha moyo wa upendo na mshikamano pamoja na jirani
zao katika medani mbali mbali za maisha.
Amewapongeza kwa kazi kubwa wanayoufanya
hata wakati mwingine bila ya kuonekana na wengi, lakini muhimu kwa ustawi na maendeleo
ya taifa la Italia. Baadhi yao ni wale wanaokumbana uso kwa uso na majanga ya maisha
katika ngazi ya kijamii, familia na mtu binafsi yanayowasilishwa kwa Rais kwa ajili
ya maamuzi na utekelezaji wake. Amewataka wafanyakazi wa Ikulu ya Italia kujenga na
kudumisha moyo wa ukarimu na uelewa kwa wote wanaokutana nao!
Jamii inawahitaji
watu wanaojisadakisha kwa weledi, utu na uelewa wa kibinadamu, daima wakionesha moyo
wa mshikamano hasa kwa wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Baba Mtakatifu
mwishoni, anawataka wafanyakazi wa Ikulu kutoka tamaa wanapokumbana na vizingiti katika
maisha na utekelezaji wa majukumu yao, bali wawe tayari kusaidiana na kutiana moyo,
ili kwa pamoja waweze kusonga mbele kwa matumaini zaidi.
Baba Mtakatifu amewahakikishia
sala zake na amewaomba kuendelea kumwombea katika maisha na utume wake, kwani anahitaji
zaidi sala za kila mmoja wao!