2013-11-14 09:35:50

Wakuu wa Jumuiya ya Madola wanakutana nchini Sri Lanka


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania ameondoka jioni ya leo tarehe 13 Novemba,2013 kuelekea Colombo , Sri-Lanka kuhudhuria kikao cha siku tatu (3) cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth Heads of Government Meeting – CHOGM) kinachotarajiwa kuanza tarehe 15-17 November,2013. Sri-Lanka inachukua uenyekiti wa Jumuiya ya Madola kwa kipindi cha miaka miwili ijayo kutoka Australia.

Pamoja na Kikao cha CHOGM Rais Kikwete anatarajia kuhudhuria kikao cha viongozi na baadhi ya wafanyabiashara . Kwa mara ya kwanza Malkia wa Uingereza hatahudhuria Kikao cha Sri-Lanka na badala yake atawakilishwa na mwanae Prince Charles.

CHOGM ni Kikao kinachofanyika kila baada ya miaka miwili ambacho ujumbe wa mwakani “Growth with Equity: Inclusive Development” ujumbe ambao unasisitiza Ukuaji na Maendeleo yatakayokuwa na faida na usawa kwa jamii nzima kwa lengo la kupunguza pengo lililopo kati ya maskini na matajiri katika jamii. Pamoja na agenda hiyo, viongozi hao watapata nafasi ya kuzungumzia hali ya kisiasa na kiuchumi katika nchi za Jumuiya ya Ulaya, mabadiliko ya hali ya hewa na biashara baina ya mataifa. Kikao cha viongozi kitafanyika baada ya kufanyika kwa baadhi ya vikao vya makundi mbalimbali katika Jumiya ikiwemo Vijana, Wafanya biashara, makundi maalum na cha Mawaziri.


Kifo cha Dkt. Mvungi chamshtusha RaisKikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kufadhaishwa na taarifa za kifo cha Mjumbe waTume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi kilichotokea Jumanne, Novemba 12, 2013 kwenye Hospitali ya Milpark, Johannesburg, Afrika Kusini.

Katika salamu za rambirambi ambazo amemtumia Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph SindeWarioba, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea kwa mshtuko mkubwa na fadhaha taarifa za kifo cha Dkt. Mvungi. “Kwa hakika ni taarifa iliyonisumbua na kunipa huzuni nyingi.” Rais Kikwete amesema kuwa hakuna shaka kuwa katika maisha yake Dkt. Mvungi ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa namna mbalimbali na kuwa kifo kimemfika wakati Taifa la Tanzania lilikuwa bado linahitaji busara, hekima na mchango wake katika mchakato mzima wa kusaka Katiba mpya.

“Kuanzia alipokuwa mwandishi wa habari katika Magazeti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Uhuru na Mzalendo, hadi uhadhiri wake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hadi uwakili katika Kampuni ya South Law Chambers, hadi uongozi wake katika Chama cha NCCR-Mageuzi, hadi uamuzi wake wa kugombea Urais wa Tanzania mwaka 2005 na sasa akiwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Dkt. Mvungi ametoa mchango wake mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Na hili hatutalisahau,” amesemaRaisKikwete.

“Kwa masikitiko makubwa, nakutumia wewe Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu nikiombeleza kifo cha Dkt. Mvungi. Nakupa pole nyingi wewe Mwenyekiti, wajumbe wa Tume na wafanyakazi wote wa Tume kwa kuondokewa na mwenzenu. Naungana nanyi kuombleza msibahuo mkubwa.”

“Aidha, kupitia kwako, natuma pole nyingi kwa wana-familia, ndugu, marafiki nan majirani wa Dkt. Mvungi kwa kuondokewa na mhimili,msimamizi wafamilia na ndugu. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa.Wajulishe kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Muhimu waelewe kuwa binafsi naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu na namwomba Mwenyezi Mungu awape subira waweze kuvuka kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake.”

Amemalizia Rais Kikwete: “Napenda kuungana nao katika kumwomba MwenyeziMungu, Mwingi wa Rehema, aiweke mahali pema roho ya Marehemu Dkt. Sengondo Mvungi. Amina.”








All the contents on this site are copyrighted ©.