Kanisa katika huduma kwa wazee wagonjwa wa mishipa ya fahamu!
Zaidi ya wajumbe 400 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanatarajiwa kushiriki katika
mkutano wa ishirini na nane wa kimataifa ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la huduma
za kichungaji kwa wafanyakazi wa sekta ya afya; mkutano unaoongozwa na kauli mbiu
"Kanisa katika huduma kwa wazee wagonjwa: tiba kwa wagonjwa walioathirika na magonjwa
ya mishipa ya fahamu.
Huu ni mkutano utakaowashirikisha wataalam wa magonjwa
ya mishipa ya fahamu, watunga sera za tiba ya magonjwa ya mishipa ya fahamu katika
karne ya ishirini na moja. Tafiti na tiba mbali mbali ambazo zimekwishapatikana hadi
sasa na matumaini kwa siku za usoni. Wajumbe watapata fursa ya kupembua kwa kina na
mapana magonjwa ya mishipa ya fahamu yanayowashambulia wazee na mahali muafaka pa
kupatia tiba.
Wataangalia mbinu mkakati wa kuzuia magonjwa ya mishipa ya fahamu
kwa wazee. Viongozi wa Kanisa watashirikisha mang'amuzi ya kitaalimungu na kichungaji
na huduma zinazotolewa na Mama Kanisa katika sekta ya afya. Mkutano huu utafunguliwa
kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Alhamisi
tarehe 21 Novemba 2013 na kuhitimishwa tarehe 23 Novemba 2013 kwa sala na tafakari.
Baadaye wajumbe hawa watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko
ambaye anaendelea kuonesha upendeleo wa pekee kwa wagonjwa kwani hawa ni rasilimali
muhimu katika maisha na utume wa Kanisa na kamwe wasisukumizwe pembezoni mwa Jamii.