Mashirika ya Misaada ya Kanisa, Majimbo, Parokia na watu binafsi waanza kuchangia
wananchi wa Ufilippini
Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko na majonzi makuu taarifa za mahangaiko
ya wananchi wengi wa Ufilippini kutokana na kukumbwa na tufani ambayo imesababisha
maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa watumiaji
wa mitandao ya kijamii, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchangia
kwa hali na mali juhudi za kuokoa maisha ya mamillioni ya watu waliofikwa na janga
hili kutokana na kukumbwa na tufani cha Haiyan kilichotokea nchini Ufilippini, hivi
karibuni. Kutokana na mwaliko huu wa Baba Mtakatifu, Mashirika ya Misaada ya Kanisa
Katoliki, Majimbo, Parokia na watu binafsi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameanza
kuchangia juhudi za kuokoa maisha ya watu walioathirika na tufani. Shirika la Kipapa
kwa ajili ya misaada kwa Kanisa hitaji limetoa kiasi cha Euro 1000,000 kama sehemu
ya mchango wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini wakati huu wanapokabiliana
na janga hili kwa wananchi wao. Umoja wa Mataifa unakaidiria kwamba, zaidi ya watu
millioni 11 wameathirika kutokana na tufani hii, watu zaidi ya 673,000 hawana makazi
baada ya nyumba zao kubomolewa kutokana na upepo na mvua kali. Maaskofu wanasema,
waathirika ni wengi zaidi ya taarifa zinavyoonesha na kwamba, ni vigumu kwa Serikali
kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi wake kwa sasa. Waathirika kwa sasa wanapata
hifadhi kwenye nyumba za Ibada, shule na viwanja vya michezo, kwani nyumba na majengo
mengi yameathirika vibaya kiasi kwamba, hayafai tena kwa matumizi ya binadamu. Shirika
la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji linasema kwamba, kwa sasa msaada uliotolewa
unalenga kukabiliana na dharura iliyojitokeza, lakini kwa siku za usoni, watajipanga
ili kuanza ujenzi wa miundo mbinu ya Kanisa katika shughuli za kiuchungaji kwa maeneo
yaliyoathirika kwa tufani ya Haiyan.