2013-11-13 09:46:15

Kumshukuru Mungu ni kuomba tena!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumanne, tarehe 12 Novemba 2013 ameongoza Ibada ya Misa ya Shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumbu kumbu ya miaka 75 tangu Rais mstaafu Benjamin William Mkapa alipozaliwa. Itakumbukwa kwamba, Rais mstaafu Mkapa alizaliwa kunako tarehe 12 Novemba 1938, Ndanda, Wilayani Masasi, Mkoani Mtwara.

Ibada hii imefanyika kwenye Parokia ya Upanga, Kanisa la Bikira Maria Immakulata, mahali ambapo Rais mstaafu Mkapa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Parokia kabla ya kuchaguliwa kuwaongoza Watanzania kama Rais wa awamu ya tatu. Hata alipochaguliwa kuwa Rais, aliendelea kusali na kushiriki pamoja na waamini wenzake kujenga Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, akawa ni mfano wa kuigwa kwa maisha adili, ukweli na uwazi, ingawa pia alikumbana na changamoto nyingi katika maisha na uongozi wake kama Rais wa Tanzania, kwani hiki kilikuwa ni kipindi cha mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini Tanzania.

Kardinali Pengo katika mahubiri yake anawaalika watanzania kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu aliowajalia watanzania. Akawasihi waendelee kuombea umoja na mshikamano a kitaifa. Kumshukuru Mungu ni kuomba tena neema na baraka zake katika hija ya maisha. Kardinali Pengo amewakumbusha waamini kwamba, wanaishi kwa nguvu, upendo na huruma ya Mungu, kumbe wanao wajibu wa kumshukuru, kama alivyofanya Rais mstaafu Benjamini Mkapa.

Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na idadi kubwa ya Maaskofu Katoliki Tanzania waliokuwa wanashiriki katika hija na ibada ya kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliofungwa nchini Tanzania, Jumapili iliyopita mjini Bagamoyo.







All the contents on this site are copyrighted ©.