2013-11-13 07:19:27

Jamani, watu wanakufa kwa baa la njaa nchini Namibia!


Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika taarifa yake kwa vyombo vya habari linabainisha kwamba, kuna watu millioni moja nchini Namibia wanaokabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame wa muda mrefu.

Ukame wa mwaka huu, haujawahi kutokea nchini Namibia katika kipindi cha miaka thelathini iliyopita. Kwa takribani miaka miwili, kumekuwepo na uhaba wa mvua hali ambayo imesababisha wakulima wengi kushindwa kulima na wafugaji kulazimika kuhama hama ili kutafuta sehemu za malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao. Idadi ya mazao ya chakula iliyovumwa ni chini ya asilimia 40%. Hifadhi ya mazao ya nafaka iliyokuwepo nchini Namibia inatarajia kumalizika mwishoni mwa Mwezi Novemba.

Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Namibia na Zimbabwe yanaendelea pia kushirikiana ili kutoa huduma kwa maelfu ya watu wanaokumbwa na baa la njaa kwa sasa. Jumuiya ya Kimataifa inashindwa kushawishika kwamba, kuna watu wanakufa kwa baa la njaa nchini Namibia kutokana na fikra kwamba, Namibia ni nchi tajiri, kumbe inaweza hata kulisha watu wake, jambo ambalo Caritas Namibia inasema, si sahihi kwani kuna watu wanakufa kwa njaa. Kuna kundi la watu wachache ambao wamebahatika kuwa na maisha bora, lakini maelfu ya watu bado wanaogelea kwenye dimbwi la umaskini.

Caritas Internationalis inaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuwasaidia wananchi wa Namibia wanaokabiliana na baa la njaa kwa sasa. Mikakati hii inaweza kwenda sanjari na maboresho ya sekta ya kilimo kwa kuangalia uwezekano wa kuanzisha mfumo wa kilimo cha umwagiliaji maji mashambani pale ambapo inawezekana, sanjari na mkakati wa upandaji miti, ili kutunza mazingira.







All the contents on this site are copyrighted ©.