Msitie chumvi mno! Haina mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amevitaka vyombo vya
habari vya Tanzania kuonyesha ukomavu katika kuisaidia nchi kujenga mahusiano na nchi
nyingine badala ya kuandika na kutangaza habari za uhusiano kwa ushabiki na utiaji
chumvi.
Wito huo wa Rais Kikwete unafuatia uandishi wa habari za mkutano kati
ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe na
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mheshimiwa Amina Mohammed uliofanyika Jumapili, Novemba10,
2013, mjini Dar es Salaam.
Baada ya mkutano huo, Waziri Amina Mohammed aliwaeleza
waandishi wa habari kuwa Kenya sasa imeelewa vizuri msimamo wa Tanzania kuhusu mchakato
wa utengamano ndani ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), hatua ambayo imepongezwa
na Rais Kikwete. Kufuatia hatua hiyo muhimu na sahihi ya Kenya, baadhi ya magazeti
yaliyochapishwa leo nchini yametoka na vichwa vya habari kama vile “Kenya yaiangukia
Tanzania” na “Kenya yasalimu amri”, vichwa vya habari ambavyo havisemi ukweli, siyo
sahihi na ni vya uchochezi na uzandiki.
Ni vichwa vya habari ambavyo haviitendei
haki Tanzania wala Kenya. Rais Kikwete hakufurahishwa, na kwahakika, amesikitishwa
na vichwa hivyo vya habari.Tanzania, kupitia hotuba ya Rais Kikwete Bungeni Alhamisi
iliyopita ilitoa hoja za kuimarisha Jumuia ya Afrika Mashariki. Kenya imeelewa hoja
hiyo ya Tanzania na imefanya uamuzi sahihi na wenye manufaa kwa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Hivyo, ni wajibu wa vyombo vya habari nchini kuchangia katika kuimarisha Jumuia badala
ya kuandika habari za utengamano kwa namna ya ushabiki usiokuwa na maana na usio na
mashiko.