"Mnanolewa ili kuendeleza dhamana na utume wa Uinjilishaji kwa Makanisa mahalia"
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu,
Jumamosi iliyopita, tarehe 9 Novemba 2013 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama
sehemu ya ufunguzi rasmi wa Mwaka wa Masomo kwa Mapadre wanafunzi wanaosoma kwenye
Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Petro, kilichoko mjini Roma sanjari na kubariki bweni
lililofanyiwa ukarabati mkubwa tayari kuanza kutumiwa na Mapadre wanafunzi kutoka
katika mataifa 42 yanayounda nchi za Kimissionari.
Katika mahubiri yake, Kardinali
Filoni amewakumbusha Mapadre wanafunzi kwamba, lengo la Kanisa kuwaleta mjini Roma
ili kupata elimu ya juu kwa kuwaaminisha mikononi mwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji
wa watu, ni kujikita zaidi katika kuendeleza kazi ya Uinjilishaji wa watu kwa ari
na kasi kubwa zaidi, kwa kuwapatia elimu bora ili waweze kutekeleza dhamana na utume
wao kwa ufanisi na tija.
Kipindi cha masomo kwa miaka miwili au mitatu ni
sehemu ya mchakato wa malezi endelevu, jambo muhimu linalokaziwa na Mama Kanisa katika
mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni kipindi cha kujiendeleza katika makuzi
ya kiroho, maadili mema na maisha ya Kijumuiya, ili kuonjeshana na kumegeana utajiri
wa mila na tamaduni kutoka katika nchi za Kimissionari. Hii ni nafasi adimu inayopaswa
kutumiwa kikamilifu na Mapadre wanafunzi wakati wote wanaponolewa hapa mjini Roma.
Kardinali Filoni anasema, Maaskofu na Kanisa kwa ujumla linapenda kuwekeza
katika majiundo makini kwa Makleri wake, ili kuendeleza kazi na dhamana ya Uinjilishaji
utume ambao Mama Kanisa anatumwa kuuendeleza hadi miisho ya dunia. Mapadre hawa wamekumbushwa
kwamba, wameitwa na Mwenyezi Mungu hata bila mastahili yao na kwamba, wote ni sawa
na wanapendeka mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kardinali Filoni anasema kwamba, Mwenyezi
Mungu amewaita na anawajalia faraja watu wake na kuimarishwa kwa nguvu na uwezo wa
Roho Mtakatifu, ili kutekeleza dhamana na utume wao ndani ya Kanisa. Anasema, Kanisa
lipo na litaendelea kuwapo kwani linahamasishwa na Kristo kwenda kutangaza Habari
Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Uinjilishaji ni sehemu muhimu sana ya utume
na maisha ya Mama Kanisa, dhamana wanayokabidhiwa pia Mapadre kuiendeleza katika Makanisa
yao mahalia.
Takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Petro mjini Roma zinaonesha
kwamba, kuna jumla ya Mapadre wanafunzi 166, kati yao kuna Mapadre 97 kutoka Barani
Afrika na 69 wanatoka Barani Asia. Kuna jumla ya Mapadre wanafunzi wapya 117 waliofika
mjini Roma kuanza mwaka wa masomo 2013- 2014.
Ibada ya misa sanjari na kubariki
bweni lililofanyiwa ukarabati mkubwa, imehudhuriwa na Askofu mkuu Savio Hon Tai Fai,
Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Askofu mkuu Protase Rugambwa,
Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa pamoja na viongozi
wengine waandamizi kutoka katika Baraza na Vyuo Vikuu vya Kipapa vilivyoko mjini Roma.
Imeandaliwa
na Padre Alfred Kwene, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Petro, Roma.