Hakuna nchi iliyopata kucharuka katika maendeleo kwa kutumia koroboi ama karabai!
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amesema kuwa Serikali yake inaelekeza nguvu
nyingi na kasi mpya katika umeme kwa sababu hakuna nchi iliyopata kuendelea kwa kutumia
koroboi ama karabai. Aidha, Rais Kikwete ametaka vyombo vinavyohusika na kusambaza
na kuunganisha umeme katika vijiji mbali mbali nchini kuongeza kasi ya kufanya kazi
kwa sababu ni lazima vijiji 1,600 vipate umeme katika muda mfupi.
Rais Kikwete
ameyasema hayo Jumapili, Novemba 10, 2013 wakati alipozungumza na wananchi katika
eneo la Buseresere/Katoro, mpakani mwa wilaya za Geita na Chato, Mkoa wa Geita ikiwa
ni mwendelezo wa ziara yake katika Mkoa wa Geita ambako amekuwepo kwa siku tatu. Buseresere
na Katoro ni miji iliyoungana lakini Buseresere iko Wilaya ya Chato na Katoro iko
Wilaya ya Geita.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza na mamia kwa mamia ya wananchi
kabla ya kuzindua mradi mkubwa wa kusambaza umeme katika vijiji vya wilaya nne za
Mkoa wa Geita na moja ya Mkoa wa Shinyanga. Umeme unasambazwa katika vijiji 14 vikiwamo
10 vya Wilaya ya Geita. Umeme huo ni sehemu ya miradi mikubwa ya miundombinu ya umeme,
barabara, maji na Uwanja wa Ndege wa Mafia inayogharimiwa na Shirika la Maendeleo
ya Milenia (MCC) la Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Milenia Tanzania (MCA-T).
Mradi
huo wa kusambaza umeme katika vijiji vya wilaya za Geita, Chato na Nyang’hwale Mkoani
Geita na Msalala (Shinyanga) umegharimu dola za Marekani 21, 477, 181 (sawa na Sh.
Bilioni 36.3) na utanufaisha wateja 3,500 katika maeneo hayo. Akizungumza katika sherehe
hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake imeamua kuelekeza nguvu nyingi katika
kusambaza umeme vijijini kwa sababu umeme ndiyo maendeleo. “Hakuna nchi iliyopata
kuendelea duniani kwa kutumia koroboi ama karabai. Nchi zote zilizoendelea zimefanya
hivyo kwa kutumia umeme na kuwekeza ipasavyo katika sekta hiyo ya umeme.”
Akijibu
malalamiko ya wananchi kuwa usambaza wa umeme huo unachelewa pamoja na kwamba wamelipia
kuunganishiwa umeme, Rais Kikwete ameziekeleza taasisi zinazohusika na kazi ya kusambaza
na kuunganisha umeme. “Mmesikia wenyewe malalamiko ya wananchi kwamba kasi ya kuunganisha
umeme siyo kubwa. Napenda tuongeze kasi kwa sababu tunayo kazi kubwa ya kusambaza
umeme katika vijiji 1,600 vya nchi yetu katika muda mfupi ujao. Hivyo, tuongeze kasi
ili tuweze kuikamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo.”
Rais Kikwete pia amewaambia
wananchi kuwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya umeme kwa urahisi, Serikali
kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imepunguza ada za kuunganisha umeme kutoka
sh. 450,000 hadi 170,000.
Mapema Jumamosi, Rais Kikwete amezindua Mradi wa
Maji wa Masumbwe katika kijiji cha Shinyanga A, wilaya mpya ambazo ziliundwa na Rais
Kikwete mwaka jana. Mradi huo uliogharimu Sh. Milioni 341 ni moja ya miradi ya maji
katika vijiji 10 kila mkoa inayogharimiwa na Benki ya Dunia (WB).
Rais Kikwete
pia amezindua Wodi ya Wazazi katika kituo cha afya cha Kijiji cha Iboya, Kata ya Mbogwe.
Mradi huo umegharimu Sh. Milioni 57 na ujenzi wa wodi hiyo ni maandalizi ya kukifanya
kituo hicho cha afya hospitali mpya ya wilaya mpya ya Mbogwe.
Naye Mbunge wa
Jimbo la Bukombe, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Profesa Kulikoyela Kanalwanda Kahigi amemsifu na kumpongeza Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuendesha nchi vizuri
na kuhangaika sana kuwaletea wananchi maendeleo. Aidha, Profesa Kahigi amemsifu Rais
Kikwete kwa kuendesha nchi kwa makini na kwa kusikiliza pande zote na kuwa mwenye
moyo wa kusaidia wananchi. Profesa Kahigi ametoa sifa na pongezi hizo Jumamosi, Novemba
9, 2013 wakati alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
eneo la Stendi ya Mabasi mjini Ushirombo, Wilaya ya Bukombe.
Katika mkutano
huo uliohutubiwa na Rais Kikwete akiwa kwenye siku yake ya pili ya ziara ya Mkoa wa
Geita, Profesa Kahigi amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi: “Namfahamu Rais Kikwete
tokea tulipokuwa pamoja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ni mtu mwenye moyo na roho ya
kibinadamu sana. Na pia napenda kumpongeza sana kwa kufanya kazi akisikiliza watu
wengine na pande zote za kisiasa za nchi yetu,” amesema Profesa Kahigi na kuongeza:
“Nawaomba viongozi ambao anawateua wawe na moyo kama wa kwake. Ni jambo la furaha
vile vile kwamba Serikali ya Rais Kikwete inatuletea umeme katika wilaya yetu ambayo
miaka na miaka hatuna umeme. Hili halina mjadala ni jambo la pongezi sana kwako Mheshimiwa
Rais kutoka kwa wana-Bukombe.”
“Ni kweli zipo changamoto na kwa kweli tutaendelea
kuzisema lakini jambo jingine zuri ni kwamba hata leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi
kwenye ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga kwa kiwango cha lami. Mnyonge mnyongeni
lakini haki yake mpeni. Rais wetu amefanya kazi nzuri sana kuwalete wananchi wetu
maendeleo.”
Mapema, Jumamosi Rais Kikwete amezindua Shule ya Msingi ya Nga’nzo
iliyoko Ushirombo, shule ambayo imedhaminiwa na ushirika wa wachimbaji wadogo wa dhahabu
wa eneo hilo la Nga’nzo na kujengwa na mwekezaji wa ndani, Ndugu Emmanuel Gungu Silanga
ambaye pia ni mwana-ushirika huo. Shule hiyo imejengwa baada ya shule ya zamani katika
eneo hilo kuwa imetishiwa na wachimbaji dhahabu wadogo ambao walikuwa wanachimba katika
eneo la shule ambako kwanza walikuwa wanachimba usiku lakini baadaye wakapat ujasiri
wa kuchimba hata nyakati za mchana.
Shule hiyo imejengwa kwa gharama ya Sh.
Milioni 460 na Rais Kikwete amewachangia wanaushirika wa wachimbaji wadogo katika
eneo hilo Sh. Milioni mbili.
Rais Kikwete Jumamosi, Novemba 9, 2013, ameweka
jiwe la msingi kwa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara nyingine muhimu ikiwa ni
barabara ya pili kuwekewa jiwe la msingi katika siku mbili za mwanzo za ziara ya Rais
Kikwete mkoani Geita. Baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya
Bwanga-Biharamulo , Ijumaa, Novemba 8, 2013, kwenye siku ya kwanza ya ziara yake,
Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi kwa kiwango cha lami la Barabara ya
Iyovu-Bwanga.
Barabara ya Bwanga-Biharamulo ambayo sherehe za uwekaji jiwe
lake ulifanyika kwenye Kijiji cha Buziku, Tarafa ya Bwanga, ina kilomita 67 na ni
barabara nyingine ambayo inaunganisha mikoa ya Kagera na Geita. Barabara hiyo inayojengwa
na kampuni ya Sinohydro ya China inagharimu Sh. Bilioni 54.76 na inatarajiwa kuwa
imekamilika Februari mwaka 2015.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi kwenye Bararaba
ya Iyovu-Bwanga zimefanyika kwenye Kijiji cha Iyovu, Kata ya Runzewe na kuhudhuriwa
na mamia kwa mami ya wananchi. Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 45 inajengwa
kwa kiasi cha Sh. Bilioni 43.36 na inatarajiwa kumalizika Agosti, mwakani, 2014.