Zimbabwe yawaambia wananchi wa Msumbiji, kupatana vinginevyo, watakiona cha moto!
Mgogoro wa kivita kati ya Serikali ya Msumbiji na Chama cha Upinzani za RENAMO umeanza
kuchukua sura mpya kwa Zimbabwe kuzitaka pande zinazohusika, kutafuta suluhu ya haraka,
vinginevyo, itauvalia njuga mgogoro huu na kutuma vikosi vyake vya kijeshi kupambana
na waasi.
Zimbabwe inahofia ikiwa kama vita ya wenyewe kwa wenyewe itafumuka
tena nchini Msumbiji, uchumi wake utazorota kwa kiasi kikubwa kwani inategemea kwa
kiasi kikubwa Bandari ya Beira kwa ajili ya kusafirishia mizigo yake. Licha ya ukweli
huu, wachunguzi wa masuala ya kijeshi wanasema kwamba, hii ni kejeli ya Zimbabwe tu,
kwani haina uwezo wala jeuri ya kupeleka vikosi vyake nchini Msumbiji kutokana na
kuendelea kukabiliana na hali ngumu ya uchumi.
Kunako mwaka 2003 Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC ilipitisha Azimio kwamba, inaweza kuingilia kati
kwa kutuma majeshi, ikiwa kama siasa na demokrasia ya nchi mwanachama iko hatarini.
Nje ya agizo la SADC, Zimbabwe, itakuwa inaingilia masuala ya ndani ya Msumbiji.