2013-11-09 08:22:04

Waamini kutoa heshima kwa masalia ya Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa kufunga Mwaka wa Imani


Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anasema, katika Maadhimisho ya Kufunga Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, waamini watapata fursa kutoa heshima yao kwa masalia yanayosadikiwa kuwa ni ya Mtakatifu Petro, Mwamba wa Imani.

Huu ni mwaliko wa kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani na kuendelea kumwabudu, daima waamini wakitambua kwamba, Uinjilishaji mpya unafanyika kwa njia ya kupiga magoti, yaani kwa njia ya sala inayomwilishwa katika matendo na ushuhuda wa maisha ya Kikristo. Waamini wanapaswa kujenga na kudumisha ari na moyo wa sala kama njia ya kujenga uhusiano wa dhati na Mwenyezi Mungu. Bila uhusiano huu, utume wowote unaofanywa na Mama Kanisa unakuwa ni kama kazi nyingine yoyote ya mshahara.

Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha maisha ya kiroho kama njia ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha, mwaliko kwa kila mwamini. Sala na kazi ni mambo msingi katika maisha ya Kikristo; mambo yanayopaswa kuendelezwa hata baada ya kufunga rasmi Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Tarehe 21 Novemba 2013, Baba Mtakatifu amechagua Monasteri moja iliyoko mjini Roma ili kwenda na kusali huko kwa faragha. Utakuwa ni muda wa kuabudu, ili kuweza kufahamu mambo msingi katika maisha, ili hatimaye, kuweza kuyakumbatia.

Askofu mkuu Fisichella anasema, Sala inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wajenge utamaduni wa kutoka na kwenda katika "Jangwa" la maisha yao ili kutafakari matendo makuu ya Mungu katika maisha yao; kwa kukuza na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani. Yesu katika maisha yake hapa duniani, alipenda kujitenga kwa ajili ya sala. Mama Kanisa kabla ya kujitosa kwa ajili ya Uinjilishaji hana budi kujikita kwanza katika maisha ya sala na tafakari ya kina.

Baba Mtakatifu Francisko atawatembelea na kusali na Wamonaki wa Camaldoli, Jumuiya ambamo wanaishi pia Watawa kutoka Tanzania. Anataka kukazia umuhimu wa Tafakari ya Neno la Mungu, huduma kwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kuwaonjesha wengine ukarimu wa kile kidogo kinachotoka katika undani wa moyo na maisha ya waamini. Waamini waitafakari sura ya Kristo kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya maskini na wagonjwa.

Kwa matukio haya, Mama Kanisa anajiandaa kwa namna ya pekee kabisa kufunga Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kwa kutoa heshima kwa masalia ya Mtakatifu Petro, Mwamba wa Imani, aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mwaka wa Imani uwachangamotishe waamini kuwa na ari na mwamko mpya katika imani tendaji inayoshuhudiwa kwa maisha adili na matakatifu. Hii ni hija inayopaswa kuendelezwa na waamini bila ya kuchoka wala kukata tamaa, kwa kutafakari uso wa Yesu Msulubiwa!







All the contents on this site are copyrighted ©.