Utume na maisha ya familia pamoja na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo!
Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia anasema kwamba,
Baba Mtakatifu Francisko ameonesha kipaumbele cha pekee kwa Familia katika utume kama
Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kuitisha Sinodi Maalum kwa ajili ya familia itakayoadhimishwa
Mwezi Oktoba 2014.
Huu utakuwa
ni wakati muafaka kwa Mama Kanisa kuweza kufanya tafakari ya kina kuhusu dhamana ya
familia, fursa zilizopo na changamoto zake katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia. Nia hii ya Baba Mtakatifu Francisko ni kielelezo cha upendo
wa dhati kwa Familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.
Askofu mkuu
Paglia anasema kwamba, Mkutano wa ishirini na moja wa Baraza la Kipapa la Familia,imekuwa
ni nafasi kwa wajumbe kuanza kunoa mawazo yao, kama sehemu ya mchakato wa maandalizi
ya Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia. Lengo ni kuliwezesha
Kanisa kuendelea kutoa mchango wake katika masuala ya ndoa, familia na zawadi ya uhai.
Familia zinakabiliwa na changamoto kubwa ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi
wa kina kwa kuibua mikakati ya kichungaji kwa ajili ya utume na maisha ya familia
katika ulimwengu mamboleo. Kuna umuhimu wa kujenga msingi wa utamaduni wa ndoa na
familia unaofumbatwa katika uelewa wa kitaalimungu na unaogusa mabadiliko msingi yanayoendelea
kujitokeza katika maisha ya watu; kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu.
Ni mwaliko kwa wanandoa kutumia nguvu zao zote
katika kujenga na kuimarisha misingi na tunu bora za maisha ya ndoa na familia, kwa
kutambua kwamba, mwanaume na mwanamke wanategemeana na kukamilishana katika dhamana
na utume wa ndoa kama Sakramenti. Askofu mkuu Paglia anasema, Roho wa Bwana anatekeleza
kazi zake hata nje ya mipaka, maisha na utume wa Kanisa, kumbe kuna uwezekano mkubwa
wa kuwa na utamaduni mpya wa maisha ya ndoa na familia hata katika ulimwengu wa utandawazi,
ambako tunu msingi za maisha ya kifamilia zinakabiliana na vitisho!
Wanawake
katika mchakato huu wana nafasi ya pekee kwani wao ndio wadau wakuu wanaotegemeza
familia nyingi duniani, kama walezi na walimu wa tunu msingi za maisha ya kiroho,
kiutu na kimaadili. Wanawake wenye imani, hekima na busara wanajenga mahusiano ya
dhati ndani ya familia zao. Bila ya kuwashirikisha wanawake kwa kina na mapana mchakato
wa Mama Kanisa kuibua mikakati mipya ya kichungaji kwa ajili ya maisha na utume wa
Familia itakwama. Wanawake ni waathirika wakubwa katika maisha ya ndoa na familia.
Pale ndoa zinapovunjika, wanawake wanalazimika kubeba mzigo wote wa familia
kwa malezi na makuzi ya watoto wao. Ni wanawake wanaokesha usiku na mchana wakiwahudumia
watoto, wazee na wagonjwa katika familia, kumbe kuna haja ya kuwatambua na kuwashirikisha
zaidi na zaidi katika maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya familia.
Askofu
mkuu Vincenzo Paglia anasema, kuna haja kwa wanaume na wanawake kuwa na utambulisho
makini kwani wanategemeana, kila jinsia ikiwa na nafasi yake katika kazi ya uumbaji.
Kanisa halina budi kutoa mwelekeo wenye mvuto na mashiko kuhusu utambulisho wa wanawake
na wanaume, kwa kutambua kwamba, linawajibu wa kurithisha imani, maadili na utu wema
kwa waamini na Jamii kwa ujumla wake. Bila familia thabiti ni vigumu kuweza kurithisha
tunu msingi za maisha kwa vijana wa kizazi kipya. Kutokana na ukweli huu, Uinjilishaji
mpya unajikita katika tunu msingi za maisha ya kifamilia.
Mama Kanisa anapotafakari
kuhusu utamaduni na mikakati bora ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia,
kuna umuhimu wa kuwashirikisha waamini walei, kwani hawa ndio wanaoguswa kwa namna
ya pekee na mipasuko, kinzani na changamoto mbali mbali za maisha ya kifamilia katika
ulimwengu mamboleo. Familia zinaposambaratika, Jamii iko mashakani. Myumbo wa uchumi
kimataifa na athari zake ni mambo ambayo yanaendelea kuathiri familia nyingi duniani
kwa kukosa uhakika wa maisha na huduma msingi. Familia zikiyumba, Jamii nyingi zinaweza
kuteleza na kuanguka!
Ni wajibu wa waamini walei kuhakikisha kwamba, kwa njia
ya ushuhuda wa maisha yao wanaenzi na kuzitegemeza familia zao. Utume huu unaweza
kutekelezwa kwa umakini mkubwa kwa njia ya vyama vya kitume vilivyo enea ndani ya
Kanisa. Askofu mkuu Paglia anasema, kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa
na kimaadili, kuna haja kwa Mama Kanisa kuwekeza zaidi na zaidi katika vyama vya kitume
kwa ajili ya malezi na majiundo endelevu ya familia, ili viweze kutekeleza dhamana
hii nyeti kwa kuwaimaarisha wanandoa katika maisha na utume wao. Wanandoa wawe na
ujasiri wa kufanya toba na wongofu wa ndani kwa makosa na mapungufu yao ya kibinadamu,
wakiwa tayari kuanza upya safari ya ujenzi wa Familia kama Kanisa dogo la nyumbani,
shule ya haki, upendo na ukarimu.
Ushauri uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican, Viongozi wakuu wa Kanisa na Nyaraka mbali mbali za Mabaraza ya
Maaskofu ni nyenzo msingi zinazoweza kulisaidia Kanisa Katoliki kuanzisha mchakato
wa mikakati ya shughuli za kichungaji kwa familia katika mapambazuko ya Millenia ya
tatu ya Ukristo. Waamini wanasubiri anasema Askofu mkuu Vincenzo Paglia kusikia Kanisa
likifafanua kwa kina na mapana kuhusu: Haki msingi za Familia, Haki ya Kazi na Mapumziko,
pamoja na Zawadi ya Uhai. Kuna changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi katika
mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo; changamoto ambazo kwa hakika zinahitaji
hekima na busara ili kufanya upembuzi yakinifu wa maisha na utume wa ndoa na familia;
Injili ya Maisha dhidi ya Utamaduni wa Kifo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.