UNITALSI ni kielelezo makini cha ushuhuda wa imani tendaji katika matendo ya huruma
kwa wagonjwa!
Miaka 110 iliyopita, ulikuwa ni mwanzo wa hija ya imani, matendo ya huruma na majiundo
makini katika maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa wagonjwa. UNITALSI, ambao ni
Umoja wa Kitaifa wa Wasafirishaji wa wagonjwa Lourdes na kwenye Madhabahu ya Kimataifa
ni juhudi zilizoanzishwa na kunako mwaka 1903 na Giovanni Battista Tomassi, wakati
alipokuwa anakaribia kukata tamaa ya maisha kutokana na kuandamwa mno na magonjwa,
aliamua kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Lourdes, Ufaransa, hapo ndipo alipoonja
matendo makuu ya Mungu katika maisha yake.
Kwa maombezi ya Bikira Maria wa
Lourdes akaongoka na hivyo kufanikiwa kuguswa na kweli za maisha ya Kikristo. Aliporudi
nchini Italia, akaandika Katiba ya UNITALSI na huo ndio ukawa ni mwanzo wa UNITALSI
kuanza kuenea kwa kasi ya ajabu nchini Italia. Hiki ni kielelezo makini cha ushuhuda
wa imani tendaji katika matendo ya huruma yanayojionesha katika Parokia na Majimbo
mengi nchini Italia.
Ni maneno ya Kardinali Tarcisio Bertone, Camerlengo wa
Kanisa Katoliki, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la
Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 9 Novemba 2013, kama sehemu ya Maadhimisho
ya Miaka 110 tangu UNITALSI ilipoanzishwa.
Tangu wakati huo, wadau mbali mbali
wameshiriki kikamilifu katika maandalizi pamoja na kuwasindikiza wagonjwa si tu katika
Madhabahu ya Kimataifa, bali hata katika hija ya maisha yao ya kila siku. Kanisa lina
kila sababu ya kumshukuru Bikira Maria msaada wa wagonjwa kwa mafanikio makubwa yaliyokwisha
kupatikana katika kipindi cha miaka 110 iliyopita.
Kardinali Bertone anasema
kwamba, kumwongokea Mungu ni mwanzo wa maisha mapya na kwamba, waamini wanapaswa kutambua
kuwa miili yao ni Hekalu la Roho Mtakatifu, kama ilivyokuwa kwa Yesu, ishara wazi
ya uwezo wa Mungu kati ya watu wake. Wagonjwa ni sehemu ya Fum bo la Mwili wa Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, katika Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu,
waamini kwa jicho la imani wanayaona Madonda Matakatifu ya Yesu kwa njia ya ndugu
zake wagonjwa, wanaopaswa kusikilizwa na wafuasi wa Kristo.
Kardinali Bertone
anasema, miaka 110 imekuwa ni ushuhuda wa wadau mbali mbali katika azma ya kusikiliza
kwa makini wagonjwa, kwa kutambua kwamba, maisha ni fumbo linalohitaji uwajibikaji
wa dhati, huruma, upendo na uvumilivu kutoka kwa kila mtu. Lakini jambo hili si rahisi
kwa watu wengi, ndiyo maana kunahitajika ujasiri unaofumbatwa katika msingi wa imani,
ili kuweza kupokea kwa matumaini magonjwa katika maisha, kwa kumuiga Kristo aliyeteseka,
akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Kardinali Bertone amewakumbusha wagonja
na wahudumu wao kwamba, ushiriki wao mkamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu ni mchakao
wa kujimwilisha katika Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Hii ni Sadaka endelevu
ya Kristo Msalabani aliyeshinda dhambi na mauti kwa nguvu ya upendo wake wa Kimungu.
Shule ya Ekaristi Takatifu inawafunda waamini kupenda na kuthamini zawadi ya uhai
hata katika hali ya magonjwa na kifo!
Kardinali Tarcisio Bertone, Camerlengo
wa Kanisa Katoliki anahitimisha mahubiri katika Maadhimisho ya Miaka 110 ya UNITALSI
kwa kuwataka wagonjwa kumkimbilia Bikira Maria ili aweze kuwaombea kwa Kristo ili
waweze kubeba pamoja na Kristo Msalaba wa mateso na mahangaiko yao.