2013-11-09 08:49:22

Sitisheni vita na anzeni mchakato wa majadiliano ya kina kwa ajili ya mafao na ustawi wa wananchi wa Msumbiji!


Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linaialika Serikali na Chama cha upinzani cha RENAMO kusitisha mapigano, chuki na uhasama na kuanza tena mchakato wa majadiliano ya kina yanayopania kujenga na kuimarisha, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa na kwamba, vita haina macho na madhara yake ni makubwa kwa maisha na mali ya watu!

RENAMO imetupilia mbali makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati yake na Serikali kunako Mwaka 1992 na hivyo kurudisha tena amani na utulivu nchini Msumbiji baada ya majanga ya vita ya wenyewe kwa wenyewe. Wananchi wa Msumbiji kwa sasa wameingiwa na hofu ya kulipuka tena kwa vita nchini Msumbiji.

Maaskofu katika mkutano wao wa Mwaka wanapenda kuonesha mshikamano wa dhati kabisa na wananchi wote wa Msumbiji bila ubaguzi na wanawataka wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda, kujenga na kuimarisha misingi ya amani sanjari na kuenzi zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Matukio ya hivi karibuni nchini Msumbiji yanaonesha kwamba, Serikali na RENAMO wameamua kupimana nguvu kwa njia ya mtutu wa bunduki, jambo ambalo ni hatari kabisa kwa ustawi, maisha na maendeleo ya wananchi wa Msumbiji. Si jambo halali kwa baadhi ya wanasiasa kutetea masilahi yao binafsi kwa gharama ya maisha ya wananchi wa Msumbiji. Maaskofu wanawaalika wananchi wote wa Msumbiji kuwa kweli ni wajenzi wa amani kwa kuheshimiana na kuthaminiana.

Amiri Jeshi mkuu wa Msumbiji pamoja na Kiongozi mkuu wa RENAMO wajitahidi kadiri ya uwezo wao kusitisha vita na kuanza mchakato wa majadiliano ya kina yanayopania kulinda na kutetea mafao ya wengi. Maaskofu wanaiomba pia Jumuiya ya Kimataifa kusaidia harakati za kupata suluhu ya amani nchini Msumbiji kwa njia za kidiplomasia, kwani kwa njia ya vita hakuna mshindi yote yanapotea na kuharibika.

Miaka 16 ya vita ya wenyewe kwa wenyewe iliwaletea wananchi wa Msumbiji majanga makubwa katika maisha kiasi kwamba, wakashuka na kubaki mkiani katika vipimo vya maendeleo kimataifa. Mkataba wa amani, uliotiwa sahihi mjini Roma kunako Mwaka 1992 umesaidia mchakato wa maboresho makubwa katika maisha ya wananchi wengi wa Msumbiji.

Wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya Msumbiji wamevutika kuwekeza na kwa sasa Msumbiji ilikuwa imeanza "kuota mbawa za maendeleo endelevu", lakini vita ya wenyewe kwa wenyewe itawashusha na kuonekana kama "soli ya kiatu"!







All the contents on this site are copyrighted ©.