2013-11-08 14:57:26

Rais Laura Nchinchilla wa Costa Rica akutana na kuzungumza na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 8 Novemba 2013 amekutana na kuzungumza na Rais Laura Nchinchilla kutoka Costa Rica ambaye baadaye pia alikutana na kuzungumza na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Viongozi hawa wawili wamefurahisha na uhusiano mzuri uliopo kati ya Kanisa na Serikali na kwamba, wamekuwa wakishirikiana kwa pamoja katika kutafuta ufumbuzi wa masuala kadhaa yanayowakabili wananchi wa Costa Rica. Kwa pamoja wameendelea kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai na utunzaji bora wa mazingira.

Kimsingi viongozi hawa wawili wamekubaliana kuanzisha mchakato utakaoimarisha uhusiano wa karibu zaidi kati ya Vatican na Costa Rica kwa ajili ya mafao na maendeleo ya pande hizi mbili. Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamegusia pia masuala ya kikanda na kimataifa kwa kutilia mkazo umuhimu wa ujenzi wa amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.