2013-11-08 11:38:24

Kwa rushwa na ufisadi watakuwa matajiri, lakini bado wataendelea kuwa watupu na watu wasiokuwa na utu!


Inasikitisha kuona kwamba, kuna wazazi wanaowalisha watoto wao chakula ambacho ni mapato ya rushwa na ufisadi unaodharirisha utu na heshima ya binadamu, kazi inapaswa kuwa ni utimilifu wa heshima ya mwanadamu. Yesu aliwaombea wafuasi wake ili wasijekutumbukia na kumezwa na malimwengu. Kuna watu ambao wamejikita katika masuala ya rushwa na ufisadi kama njia halali ya kujipatia pato la maisha yao.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu aliyoadhimisha kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, siku ya Ijumaa, tarehe 8 Novemba 2013. Anasema, Mwenyezi Mungu anawataka wanadamu kutoka jasho la halali ili kujipatia mahitaji yao msingi. Tamaa ya mali na utajiri wa haraka haraka unaoanza kwa rushwa ndogo ndogo, umewapelekea watu wengi kujikuta wamekuwa ni mafisadi wa kutupwa, mambo ambayo wakati mwingine yanawatumbukiza hata katika biashara haramu ya dawa za kulevya, hali inayosababisha majanga kwa vijana wengi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga msingi wa uaminifu, kwa kuthamini na kuenzi kazi halali; daima wakitegemea maongozi ya Roho Mtakatifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amesali na kuwaombea watoto na vijana wanaopokea mahitaji yao msingi kutokana na fedha ya rushwa na ufisadi unaofanywa na wazazi pamoja na walezi wao.

Watambue kwamba, utu na heshima ya binadamu vinapata chimbuko lake katika kazi halali na wala si katika njia za mkato. Mwanadamu hapa duniani ni mpita njia, daima anatembea na Fumbo la kifo katika hija ya maisha yake. Kwa rushwa na ufisadi watakuwa matajiri, lakini bado wataendelea kuwa watupu na watu wasiokuwa na utu!







All the contents on this site are copyrighted ©.