Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania?
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukuletea hotuba ya Rais Jakaya Kikwete
wa Tanzania aliyoitoa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Dodoma, tarehe
7 Novemba 2013. Kwa kifupi amezungumzia kwa undani kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki
na nafasi ya Tanzania; operesheni tokomeza inayopania kulinda wanyama pori katika
hifadhi za taifa. Ushiriki wa Tanzania katika jeshi la Umoja wa Mataifa ili kulinda
na kudumisha amani nchini DRC pamoja na rasimu ya pili ya Katiba inayotarajiwa kukamilika
hapo tarehe 15 Desemba 2013. Sasa unaweza kuzama zaidi katika hotuba hii!
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili niweze kuzungumza
na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa uhai, ustawi na maendeleo
ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika; Nimeambiwa kuwa taarifa
ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge, kumekuwepo na dhana
mbalimbali. Wapo waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya
na hasa matukio ya wiki chache zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni
Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja kuwakaripia Waheshimiwa
Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni
hii muhimu. Na wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya
Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa
Spika; Hayo si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu
ni kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya
hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai niliyopewa
kuwa niyasemee japo kidogo. Nimeona ni vyema nifanye hivyo. Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji
wake. Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua
ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia walishatoa
Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba. Kinachosubiriwa
kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo
tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika; Kwa
upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu yatakayowezesha
mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata. Jambo la kwanza ni kutungwa
kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake. Baada
ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili
kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho.
Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo
wote mwakani, tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea
kufanya tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika
kwa mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa sikukasirishwa
na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji
haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli
hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.
Mheshimiwa
Spika; Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa
kuwa takribani 350,000. Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya
1970 na 1980 ilipofika mwaka 1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000 tu. Ilipofikia
hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na kuongozwa
na Meja Jenerali John Walden (ambaye sasa ni marehemu) kuendesha mapambano dhidi
ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya
wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka (CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe
za ndovu duniani, idadi ya ndovu nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.
Tumewaomba
Fankfurt Zoological Society ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori kwa
miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote nchini
ili tujue hali halisi ikoje. Kazi hiyo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu
na faru nchini na kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo. Idadi
kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko
duniani inathibitisha ukweli huo. Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba, 2013,
hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo
11,212 na vipande 22 vya pembe za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978 vilikamatwa.
Aidha, katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea Tanzania
vyenye uzito wa kilo 17,797 vilikamatwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru
lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao. Nchi za Gabon, Kenya, Afrika
ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe, Zambia na nyinginezo nazo
zinakabiliwa na matatizo kama yetu. Tatizo limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya
ya Kimataifa kushtuka na kuamua kuingilia kati kwa namna mbili. Kwanza kuunga mkono
juhudi za uhifadhi wa ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao. Na, pili, kuchukua
hatua thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio wazi kuwa
kama hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha Operesheni
Tokomeza ni sahihi kabisa. Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka
1989 yanatupa imani kuwa na safari hii pia tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama
hii sasa ni sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini.
Hakika wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia itatuhukumu
vibaya.
Mheshimiwa Spika; Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu
kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi
kuwa tutayafanyia kazi. Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda
wa kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu na wale
wasiokuwa waaminifu wataondolewa. Halikadhalika, kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa
ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe kwa mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa
Spika; Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa
mifugo iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa
wenye mifugo na mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote hizo zitafanyiwa
kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo. Pamoja na hayo, napenda kuwakumbusha
ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa
katika maeneo ya hifadhi.
Naomba tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza wajiepushe
na kufanya hivyo. Ni uvunjifu wa Sheria za nchi. Naomba pia, wananchi waelimishwe
ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu
iliyotamkwa kwenye sheria. Hivyo tusiwalaumu wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa
ni watu wabaya. Wanatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge hili. Pale wanapotenda
visivyo tuseme, watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo Mheshimiwa
Spika; Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie
kikosi kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza
nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la
msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda
mrefu kutokana na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
Tulikubali, kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi kama
hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu. Ni miezi saba (tangu Aprili)
sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza majukumu yao vizuri
tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa inatolewa
na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa
Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu wa Serikali ya Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili. Yapo yanayopewa
jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi wake huwa hawapewi majukumu ya kimapigano na
hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa kujihami tu. Kwa kawaida majeshi yenye jukumu
hili hupelekwa mahali ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano. Wanapelekwa
kusaidia kuona Mkataba unatekelezwa ipasavyo.
Aina ya pili ni ile ya majeshi
yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua hatua za
kufanya amani ipatikane. Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi
dhidi ya wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo. Maana yake
ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu au vikundi vinavyovuruga
amani. Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza, wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye
hatari zaidi ya kupoteza maisha au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao
wameuawa na kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika; Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo
chini ya utaratibu huu wa pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi
kama hapana budi kufanya hivyo. Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa
na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu shupavu. Daima
tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola
awape mapumziko mema. Ameen.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia
nafasi hii kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio
ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23. Tunamtakia yeye na
wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo
hilo na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu wa Kongo. Pia nawapongeza sana
wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha
mafanikio kupatikana. Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi
wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ.
Jumuiya
ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika; Kama nilivyosema
awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wabunge wetu. Nimeyachomekea tu kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati
tulio nao. Jambo lililonileta hapa leo ni kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika Jumuiya hiyo. Nimeona nifanye hivyo
kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio ya hivi karibuni
ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda
na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi. Viongozi wenzangu
hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe, Uganda;
tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali,
Rwanda.
Mheshimiwa Spika; Naomba kwanza niweke wazi jambo moja,
kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano
katika kufanya mambo mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo
na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini, nchi wanachama zinatakiwa
kufanya hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba
hayamo katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au
taasisi za Jumuiya kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo
yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote iliyokuwa
tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi nyingine.
Mheshimiwa
Spika; Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada
ya mikutano hiyo, kuna mambo yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi
hizo kwa lengo la kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Mambo hayo ni haya yafuatayo: (1) Kujenga reli ya kisasa
kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura. (2) Ujenzi wa Bomba
la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini. (3) Kujenga
Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda. (4) Kuanzisha Himaya Moja
ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote; (5)
Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu
ya Katiba ya Shirikisho. (6) Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja
ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
(7) Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati
ya kusafiria katika nchi zao; na (8) Kuongeza uzalishaji na usambazaji
wa umeme.
Mheshimiwa Spika; Ni dhahiri kwamba orodha hiyo
imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano,
mambo manne kati ya hayo manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha
au kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na
usambazaji wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja ya
nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado jukumu la kuzalisha na
kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua. Lakini, hivi ndugu
zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa
na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?
Jambo la pili,
ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda. Hili si suala la Jumuiya
bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine.
Rais Yoweri Museveni alituarifu mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa
tutapata mafuta karibu na nyumbani. Alitualika kushiriki katika ujenzi wake sijui
sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika; Jambo
la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda.
Hili si jambo linalobanwa na masharti ya Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua
kufanya ili kuwezesha mafuta yao kufika kwenye masoko. Hata hivyo, nimeambiwa kuwa
Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi
kuwa nalo lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Inaelekea
mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba hilo. Mheshimiwa
Spika; Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali
– Bujumbura. Hili nalo hatuna tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
ni jambo lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika. Hata hivyo, ni vyema kutambua
ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi
za Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa
na Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East
African Railway Masterplan, tuna East African Road Network, na tuna Lake Victoria
Development Programme kwa ziwa Victoria. Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli
ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli hiyo na
reli ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea
hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki ambapo naamini Tanzania
ni mdau muhimu. Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo sivyo.
Mheshimiwa
Spika; Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini
wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28,
2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano
wa Afrika Mashariki kwa kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa
Spika; Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa
utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno
nayo. Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na
Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa
tayari waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha
(Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka
uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika; Katika Mkutano Maalum
wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28 Aprili, 2012 Jijini Arusha,
tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single
Customs Territory). Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi mwanachama itasimamia
shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato yake kama ilivyo sasa. Hata hivyo,
kwa bidhaa zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji
wa mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia. Mapato hayo
yatawasilishwa kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka.
Mheshimiwa Spika; Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza
la Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji
wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano wa 15 wa Wakuu
wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba, 2013. Iweje leo nchi tatu
wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza? Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye
hivyo?
Mheshimiwa Spika; Kuhusu Shirikisho la Kisiasa
la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana na hii ya Himaya ya Forodha. Katika Mkutano
wa 14 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea
taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho.
Mkutano huo uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia
Shirikisho la Kisiasa na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na
Timu ya Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha mapendekezo
ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi mwezi Novemba, 2013. Iweje
leo wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika; Kwa kweli huwa najiuliza maswali
mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa na viongozi wenzangu watatu
na kwa nini! Nakosa majibu ya uhakika. Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika
Mashariki na je wanataka kuunda yao? Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia
vitimbi tutoke! Au sijui wanachuki na mimi! Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge
kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa). Tupo na tutaendelea
kuwepo!
Mheshimiwa Spika; Tanzania haijafanya jambo lo lote
baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote mwanachama. Na ukweli ni kwamba ni mwanachama
mvumilivu, mtiifu na mwaminifu kwa Jumuiya. Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya
na kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Sabahu ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke
yao kwa kweli haieleweki.
Mheshimiwa Spika; Tunasikia eti kuwa baadhi
yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa
tayari tutajiunga. Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing).
Hivi ni nani hayuko tayari (who is not willing?) Haiwezekani watu waitane wenyewe
bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi
wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari. Madai hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme
ukweli. Kama walitualika tukakataa ndiyo wanaweza kusema hayo.
Mheshimiwa
Spika; Kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba Tanzania haina
moyo wala dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano wa Afrika Mashariki. Kwa sababu
hiyo inasemekana eti nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na kwamba Tanzania tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai
kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo
yamekuwa yanarudiwa au kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa
Afrika Mashariki na hata kwingineko duniani waamini hivyo.
Mheshimiwa
Spika; Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana ukweli wo
wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha ukweli wake hazina mashiko.
Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania walivyo. Tanzania ni muumini wa
dhati wa umoja na utengamano wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika. Tumethibitisha
hivyo kwa vitendo kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
na Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda mrefu kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa Spika; Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki
zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo ambalo hatujalifanya
ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa sababu ya kupuuza Jumuiya.
Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele cha juu. Hatuwezi kuhangaika kwa
gharama kubwa ya muda wetu, fedha zetu na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha,
kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda
na kudhoofisha maendeleo na ustawi wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii
akilini. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.
Mheshimiwa Spika;
Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira,
uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa sahihi juu yetu. Mimi siamini
kama kuna mengine. Hata hivyo, napata taabu kuamini kwamba kutofautiana kwa mawazo
katika mambo hayo kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende hata kushirikiana nasi kwa
mambo ambayo hayana matatizo na tumekuwa tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa
Spika; Tanzania imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya yetu hatua
moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatuna tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote.
Tusiende kasi ya kupindukia. Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia
Soko la Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa
Spika; Ni kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa
kabla ya kukamilisha baadhi ya hatua. Na, tulifanya hivyo kwa nia njema ya kutaka
Shirikisho lijengwe juu ya msingi imara. Na, msingi huo si mwingine bali utengamano
wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Kifedha zilizojengeka
vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha wanachama wote sawia.
Mheshimiwa
Spika; Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo
kikubwa cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kama mambo
ya kiuchumi yakipangika vizuri na kila nchi ikanufaika sawia, unajenga msingi imara
kwa Shirikisho la Kisiasa kustawi na kudumu. Kama ngazi hizi tatu za awali hazitashughulikiwa
vizuri na nchi wanachama zikahisi hazinufaiki ipasavyo, Shirikisho litayumba au kuyumbishwa
hivyo kudumu kwake kutakuwa kwa mashaka.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe
moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja. Kwa msimamo na mtazamo wetu, Shirikisho
iwe ndiyo hatua ya mwisho. Na huo siyo msimamo wangu au wa Serikali peke yake, ndiyo
msimamo wa Watanzania walio wengi. Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa
mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi
kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa
hapa nchini Kamati hiyo iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake,
Kamati ilieleza kuwa asilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho
lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake.
Mheshimiwa
Spika; Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu
kuwepo kwa Shirikisho na kasi ya utekelezaji wake. Watanzania wengi sana wanaunga
mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka jambo hilo lisifanywe
haraka haraka. Wanataka lifanywe kwa umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama
ilivyoainishwa katika Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa
Spika; Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inakwenda sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana tumeafiki mapendekezo
ya Kamati ile ya mwaka 2004 iliyoongozwa na Mheshimiwa Amos Wako wakati ule akiwa
Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya kuharakisha
utekelezaji wa mchakato wa utengamano wa Afrika Mashariki. Mkataba wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya Umoja wa Forodha
lakini uko kimya kuhusu ngazi zilizofuata. Ili kuondoa kasoro hiyo na kwa nia ya
kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni na mapendekezo juu ya
namna ya kufanya hivyo. Kamati ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na hisia za watu
wa makundi mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu ujenzi wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa
Spika; Kwa upande wa Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako
ilitambua hisia za Watanzania kuhusu ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo
yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama kuamua. Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati
ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka ufike
ukomo wake wa miaka mitano. Baada ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza
kupunguzwa. Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya kuunda Soko la Pamoja yaanze
hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa
Soko la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara baada ya ngazi hiyo kuanza matayarisho
ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha yanaanza. Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho
ya kuunda Shirikisho yanaanza. Kamati pia imetoa mapendekezo ya namna ya kufikia
uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa nchi wanachama wataamua kwa kura. Tukifuata
mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama tufanyavyo sasa Tanzania
haina matatizo nayo.
Mheshimiwa Spika; Baada ya kazi kubwa na
nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wa Jumuiya yao inasikitisha
kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa
kazi na kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi pale watu wanapobagua wenzao na wanapofanya
mambo yanayopingana na Mkataba wa Jumuiya na Itifaki zake. Kwa kweli kama mwenendo
huu hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele ya safari.
Mheshimiwa Spika; Nchi
yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo imara na iliyo
endelevu. Jumuiya ambayo inaendeshwa vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama
na watu wake wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia. Tanzania haina tatizo na kuharakisha
mchakato wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla hazijakamilika.
Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila hatua tunayochukua. Bila ya kufanya hivyo,
Jumuiya yetu itakuwa imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa
na changamoto nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya
ya Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia matakwa
ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya kila tuwezalo
kuhakikisha kuwa Jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe
hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake. Ndiyo maana,
hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
inaendelea kustawi.
Tutaendelea kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo
yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa kuheshimu
matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na maamuzi halali
ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu wake kama yalivyo malengo
na madhumuni ya kuundwa kwake.
Mungu Ibariki Afrika Mungu Ibariki Tanzania Idumu
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge;
Asanteni sana kwa kunisikiliza.