2013-11-08 10:14:47

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapania kufanya hija ya pamoja!


Wajumbe wa mkutano wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliofunguliwa hapo tarehe 30 Oktoba 2013, huko Busan, Korea ya Kusini, kufungwa rasmi siku ya Alhamisi, tarehe 8 Novemba 2013, wameyataka Makanisa wanachama kutembea kwa pamoja katika mshikamano wa kidugu. Mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni hufanyika kila baada ya miaka 7 hadi 8 ili kuweka mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Makanisa 345 ambayo ni wanachama wa Baraza hili.

Ujumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni mara baada ya maadhimisho ya mkutano wake mkuu, unayataka Makanisa wanachama na Wakristo katika ujumla wao kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai, kwa kudumisha misingi ya haki na amani, Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza kwani Yeye ni Mungu wa uhai.

Kunako mwaka 1948 Baraza la Makanisa Ulimwenguni lilituma ujumbe kwa Makanisa wanachama, kuwakumbusha kwamba, walipania kuishi na kutembea kwa pamoja. Ujumbe wa Mwaka 2013 unakazia tena lengo waliokuwa wamejiwekea wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mkutano wao mkuu uliofanyika mjini Amsterdam, kwa kuwaalika Wakristo kuendeleza mchakato wa hija ya haki na amani, kwa kutemba kwa pamoja!

Wajumbe wanakazia umuhimu wa umoja na mshikamano kati ya Makanisa na Jamii ya watu, ili kushirikishana utajiri na rasilimali ya dunia, ili kuganga: njaa, vita na magonjwa. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na watu wote wanaoendelea kusimama kidete kutafuta misingi ya haki na amani!







All the contents on this site are copyrighted ©.