Baba Mtakatifu Francisko asikiliza na kujibu kilio cha wananchi wa Kenya!
Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki,
Cor Unum, hivi karibuni alizindua Hospitali inayomilikiwa na kuendeshwa na Shirika
la Masista wa Katekesi wanaotekeleza utume wao Jimboni Eldoret, nchini Kenya.
Sherehe
hizi zimehudhuriwa na Askofu mkuu Charles Daniel Bavo, Balozi wa Vatican nchini Kenya
pamoja na viongozi wa Kanisa kutoka Jimboni Eldoreti. Hizi ni juhudi za Baba Mtakatifu
Francisko kuhakikisha kwamba, Kanisa linasikiliza kilio cha maskini na kujitahidi
kujibu kwa njia ya matendo ya huruma kama kielelezo cha imani tendaji.
Katika
mahojiano na Gazeti la L'Osservatore Romano linalomilikiwa na kuendeshwa na Vatican,
Monsinyo Segundo Tejado Munoz, Katibu mkuu msaidizi wa Cor Unum anasema, Baraza hili
ni kielelezo cha mshikamano wa upendo unaooneshwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa
watu wanaokabiliana na majanga mbali mbali ya maisha, pamoja na kusaidia mchakato
wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la umaskini, ujinga na maradhi.
Huduma
ya upendo wa Baba Mtakatifu inachangiwa na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki
kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa Katoliki limeendelea kuwa ni mdau mkubwa
katika maboresho ya huduma ya afya ya jamii kwa miaka mingi. Hii ni sehemu ya Uinjilishaji
wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kama alivyowahi kusema Papa Paulo wa sita.
Huduma ya afya inayotolewa na Kanisa Katoliki Barani Afrika inajikita zaidi
vijijini, huduma kwa mama na mtoto, wazee na hasa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.
Hii ndiyo picha inayojionesha pia Jimboni Eldoreti, nchini Kenya. Hospitali ya Trinity
Mission Hospital iliyoko Jimboni humo pamoja na mambo mengine inapania kutoa huduma
kwa Jamii ya wafugaji ambayo inakabiliana na changamoto nyingi za huduma za Kijamii.
Mradi wa Hospitali hii ni cheche za matumaini kwa wananchi wa Eldoreti kama
kielelezo cha mshikamano na maskini katika mapambano dhidi ya magonjwa bila ugabuzi.
Cor Unum inasema, Bara la Afrika bado linaendelea kuhifadhi tunu msingi za maisha
ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinazoweza kuhamasisha mchakato wa Uinjilishaji mpya
sehemu mbali mbali za dunia. Barani Afrika familia inayoundwa kati ya Bwana na Bibi
bado inapewa kipaumbele cha kwanza, ikilinganishwa na "majanga" yanayoendelea kujitokeza
Barani Ulaya na Amerika.
Afrika bado inaendelea kujikita katika utamaduni
wa maisha, licha ya utamaduni wa kifo unaoanza kujipenyeza kwa njia ya sera za utoaji
mimba kama sharti la kupokea misaada ya maendeleo ili kupambana na umaskini. Baba
Mtakatifu Francisko ana matumaini makubwa kwa Kanisa Barani Afrika na kwamba, litaendelea
kuchungia kwa hali na mali katika maendeleo na ustawi wa Kanisa la kiulimwengu licha
ya changamoto zilizoko mbele yake.
Misimamo mikali ya kidini na vitendo vya
kigaidi ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kusimamiwa kidete ili kuhakikisha kwamba,
haki msingi za binadamu zinalindwa na kuheshimiwa; watu wanaweza kutekeleza uhuru
wa kuabudu bila woga wala wasi wasi wa kuvamiwa. Mashambulizi ya kidaidi yanaendelea
kujenga hofu na wasi wasi miongoni mwa wananchi wengi Barani Afrika.
Mauaji
ya kinyama yaliyofanyika Westegate, mjini Nairobi na kupelekea zaidi ya watu 60 kupoteza
maisha ni jambo la kusikitisha sana. Madhulumu ya kidini bado yanaendelea pia kujionesha
nchini Somalia na Tanzania, nchi ambayo kwa miaka mingi ilifurahia amani, utulivu
na mshikamano wa kitaifa, kwa sasa misingi hii inaanza kusambaratika taratibu kadiri
siku zinavyokwenda!
Cor Unum inayapongeza Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki
yanayotekeleza dhamana na wajibu wake katika kambi za wakimbizi zilizoenea sehemu
mbali mbali za Afrika, lakini kwa namna ya pekee nchini Kenya. Kambi ya Wakimbizi
ya Dadaab, iliyokuwa na uwezo wa kutoa hifadhi kwa wakimbizi 90, 000 kwa sasa inahifadhi
watu zaidi ya 450,000. Hii ni kambi kubwa ya wakimbizi kuliko zote duniani. Kambi
hii inakabiliwa na changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa
kwa kushirikiana na wadau mbali mbali.
Ukame wa kudumu Kaskazini mwa Kenya
ni changamoto nyingine katika kuwahudumia wakimbizi. hali ya usalama kwa wafanyakazi
wa Mashirika ya Misaada Kitaifa na Kimataifa si shwari sana kwani kila wakati wanakabiliana
na kifo mbele yao! Kanisa Katoliki nchini Kenya linatekeleza wajibu wake barabara
katika medani za kidiplomasia na utoaji wa misaada ya kiutu katika mchakato wa kutafuta
suluhu ya kudumu na kwa ajili ya mafao ya wengi!