2013-11-07 10:59:50

Wivu na unafiki ni sumu kali inayoweza kumzuia mwamini kuonja: furaha, huruma na mapendo ya Mungu


Kuna furaha isiyokuwa na kifani kwa Mwenyezi Mungu pale mdhambi anapotubu na kumwongokea Mungu ili kuonja tena huruma na upendo wake wa kibaba, uliojidhihirisha kwa namna ya pekee kwa njia ya Yesu Kristo, aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa wadhambi, ili waweze kutubu na kumwongokea tena Mungu.

Mwelekeo huu wa maisha na utume wa Yesu, ulimfanya kuonekana kuwa ni mtu wa hatari katika Jamii kwani alikuwa anashirikiana kwa karibu zaidi na wadhambi. Kwa baadhi ya watu hii ilikuwa ni kashfa kwani Yesu alikuwa anakwenda kinyume cha dhamana na utume wa Nabii. Lakini hii yote ni Litania ya maisha ya unafiki yaliooneshwa kwa namna ya pekee na Mafarisayo. Yesu anajibu mapigo kwa simulizi la furaha kwa: mwanakondoo aliyepotea na shilingi iliyoonekana; kielelezo cha Mwenyezi Mungu asiyechoka kuwatafuta waja wake usiku na mchana hadi pale atakapowaonjesha tena: furaha, huruma na upendo wake wa kibaba!

Hii ni sehemu ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko, aliyoyatoa kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, siku ya Alhamisi, 7 Novemba 2013. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutambua kwamba, wanaweza kukimbia na kutoweka mbele ya huruma na upendo wa Mungu, lakini bado wanabaki kuwa ni sehemu ya Watoto wa Mungu, walioumbwa kwa sura na mfano wake; wote wanapaswa kuonja tena furaha inayobubujika kutoka kwa Mungu.

Mwenyezi Mungu anafurahia pale mdhambi anapotubu na kuongoka; pale anapoacha njia zake mbovu na kuanza kukumbatia furaha, huruma na upendo wa Mungu. Wivu na unafiki ni sumu kali inayoweza kumzuia mwamini kuonja furaha, upendo na huruma ya Mungu. Hata katika dhambi, Mungu anatoa bado nafasi kwa mdhambi kutubu na kumwongokea! Huyu ndiye Baba mwenye huruma na mapendo!







All the contents on this site are copyrighted ©.