Mtumishi wa Mungu Maria Teresa Bonzel kutangazwa kuwa Mwenyeheri, hapo tarehe 10 Novemba
2013
Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa
wenyeheri na watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ijayo tarehe
10 Novemba 2013, anatarajiwa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Maria Teresa Bonzel kuwa
Mwenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa Jimboni Paderborn, Ujerumani.
Mtumishi
wa Mungu Maria Teresa Bonzel alizaliwa na kulelewa katika familia ya Kikristo. Wazazi
wake walikuwa ni wachamungu na mfano bora wa kuigwa na jirani, kwani walijitahidi
kujenga familia yao, ikawa ni Kanisa dogo la nyumbani, shule sala na utakatifu wa
maisha.
Baada ya masomo yake ya msingi, "Aline" kama walivyozoea kumwita nyumbani
kwao, alitamani sana moyoni mwake kuwa mtawa, lakini akakumbana na pingamizi kutoka
kwa mama yake mzazi aliyekataa kuridhia ndoto yake na kwamba, dada yake alikuwa pia
ni mgonjwa. Mahangaiko haya ya ndani yaliandamana naye katika safari ya maisha yake
ya kiroho, hadi pale alipoaga dunia.
Mtumishi wa Mungu Maria Teresa Bonzel
hakukata wala kukatishwa tamaa, aliendelea kubaki mwaminifu kwa ndoto yake ya kutaka
kuwa mtawa kwa ajili ya Mungu na jirani zake. Kunako mwaka 1863 Askofu wa Jimbo la
Paderborn, Ujerumani aliridhia wazo la Maria Teresa Bonzel na wenzake kuanzisha Shirika
la Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisko.
Shirika hili jipya likaitwa "Masista
Fukara Wafranciskani Waabudu wa Daima". Sr. Bonzel alichaguliwa kuwa Mama mkuu wa
Shirika hadi alipofariki dunia tarehe 6 Februari 1905. hadi kufariki kwake, Shirika
lilikuwa na watawa 870 waliokuwa wanaishi katika nyumba 71 nchini Ujerumaini. Amerika,
Shirika lilikuwa na watawa 700 waliokuwa wanaishi katika nyumba 42.
Maisha
ya mtumishi wa Mungu Maria Teresa Bonzel yalisimikwa katika sala iliyomwilishwa kwenye
matendo ya huruma anasema Kardinali Angnelo Amato. Ni mtawa aliyejiachilia mikononi
mwa Mwenyezi Mungu wakati wa majanga ya maisha; wakati wa shida na karaha. Alikuwa
na Ibada ya pekee kabisa kwa Yesu wa Ekaristi Takatifu, akaonesha upendo usiokuwa
na mipaka kwa watoto waliokuwa wanaishi ndani na nje ya taasisi yake. Alihakikisha
kwamba, watoto wengi zaidi wanapata hifadhi na usalama katika maisha yao kwa kuwakabidhi
kwenye familia bora.
Mwenyeheri Maria Teresa Bonzel ni zawadi kubwa si tu kwa
Shirika na Jimbo lake la Paderborn, bali hata kwa Kanisa zima, kwani ni kielelezo
cha moyo uliokumbatia kwa dhati kabisa maneno ya Kristo, kiasi cha kuchanua na kutoa
harufu safi ya ujasiri na utakatifu wa maisha unaojionesha katika imani tendaji. Lengo
la kuwekwa kwake wakfu, lilikuwa ni kumsaidia katika mchakato wa kutafuta utakatifu
wa maisha kwa kukumbatia Mashauri ya Kiinjili; muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu.
Ni mtawa anayeonesha jitihada za mwanadamu katika kumtafuta na hatimaye, kukutana
na Mwenyezi Mungu, kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zake
wanaohitaji zaidi msaada wake. Na kwanjia hii akabahatika kufikia utimilifu wa maisha
yake.
Hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko alisema kwamba, watakatifu kabla
ya kuvishwa taji la utukufu na heshima, walikuwa ni watu wa kawaida, waliokumbuna
na majanga, furaha na matumaini katika maisha yao ya kila siku. Ni watu walioonja
upendo wa Mungu uliowawezesha kuleta mageuzi katika maisha yao, wakaamua kujitosa
kimasomaso kwa ajili ya Mungu na jirani; wakasambaza harufu nzuri ya matendo ya huruma,
furaha na amani.
Waamini wanakumbushwa kwamba utakatifu wa maisha si upendeleo
kwa ajili ya watu wachache, bali ni wito na mwaiko kwa wote. Sakramenti ya Ubatizo
inamkirimia mwamini neema katika imani, matumaini na mapendo; ili kukua na kukomaa
katika utimilifu wa maisha ya Kikristo, kwa kupokea na kutekeleza mapenzi ya Mungu
katika hija ya maisha yake ya kila siku! Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya kila
mwamini anasema Kardinali Angelo Amato.