2013-11-07 11:26:01

Matendo ya huruma ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili


Uhusiano kati ya imani, matendo ya huruma na Uinjilishaji; dhamana ya Askofu na Waamini katika kushuhudia imani kwa njia ya ukarimu kwa kutambua kwamba, Yesu amezaliwa maskini ili kuwainua wanyonge kutoka katika unyonge wao ni kati ya mambo muhimu yaliyojadiliwa na wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya wanaojihusisha na huduma ya utoaji wa misaada kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, katika mkutano wao uliofunguliwa hapo tarehe 4 hadi tarehe 6 Novemba, huko Trieste, Italia.

Mkutano huu ulikuwa umeandaliwa na Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum pamoja na Shirika la Misaada la Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya. Mkutano huu umehudhuriwa na viongozi wakuu kutoka Cor Unum na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, ambao kwa pamoja wamejadili kwa kina na mapana Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita unaojadili kuhusu huduma ya upendo kama asili ya Kanisa.

Wajumbe hawa wamesikiliza shuhuda mbali mbali zilizotolewa na wadau katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; dhamana inayotekelezwa kwa kusukumwa na imani katika matendo. Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki yanapaswa kuthamini utambulisho wake wa Kikanisa yanapotekeleza utume wake. Parokia na Familia za Kikristo ziwe ni mashahidi wa upendo kwa maskini na wahitaji zaidi.

Huduma zinazotolewa na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki zinaweza kuwa ni kielezo na kikolezo cha mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Kwa njia hii, Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuonesha moyo wa ukarimu ili kukidhi mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Jumuiya ya waamini ioneshe imani yake katika matendo.







All the contents on this site are copyrighted ©.