2013-11-07 15:35:34

Dr. Mvungi yuko Afrika ya Kusini kwa matibabu zaidi!


Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dr. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) amesafirishwa Alhamisi, Novemba 7, 2013) saa 5:45 asubuhi kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi. Akiwa nchini Afrika Kusini, Dr. Mvungi atapata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo Jijini Johannesburg.

Itakumbukwa kuwa Dr. Mvungi alivamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013. Tukio hilo la uvamizi linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

Tangu siku alipojeruhiwa, Dr. Mvungi alikuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI). Hata hivyo, Madaktari waliokuwa wakimtibu MOI, walishauri afanyiwe uchunguzi na matibabu zaidi. Dr. Mvungi ameondoka na ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Flightlink na ameambatana na Dr. Mugisha Clement Mazoko kutoka MOI; Muuguzi Bi. Juliana Moshi; na mtoto wa kaka yake Bw. Deogratias Mwarabu. Serikali inagharamia gharama zote za matibabu ya Dkt. Mvungi.

Tume inawaomba wananchi wote waendelee kumuombea kwa Mungu Dr. Mvungi ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida na hatimaye kuendelea majukumu yake.









All the contents on this site are copyrighted ©.