2013-11-07 10:40:25

Changamoto katika mchakato wa kupambana na lishe duni!


Kikosi kazi cha Baraza la Kipapa la Taasisi za Sayansi hivi karibuni limehitimisha mkutano wake maalum uliokuwa unajadili pamoja na mambo mengine kuhusu: elimu, teknolojia za kibayolojia, utamaduni mintarafu huduma kwa zawadi ya uhai kama sehemu ya mchakato wa kupambana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha unaoendelea kusababisha majanga sehemu mbali mbali za dunia.

Mkutano wa Kikosi kazi, umeongozwa na kauli mbiu "Mkate na Akili. Elimu na Umaskini". Wajumbe wamepata fursa ya kupembua madhara yanayosababishwa na umaskini katika mchakato wa maendeleo endelevu mintarafu akili ya binadamu, jambo ambalo linapaswa kushughuliwa na wadau mbali mbali. Hapa wanasayansi wa afya ya akili, wachumi, wanabayolojia na waelimishaji, walitoa mchango wao kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mwanadamu.

Baa la umaskini ni kati ya changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hali hii inagumishwa pia na lishe duni; jambo linalohitaji mbinu mkakati katika uzalishaji, uvunaji, usambazaji na ulaji pamoja na kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wakulima wadogo wadogo ambao mara nyingi wananyonywa kwa kupewa bei ndogo ya mazao sokoni. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yasaidie pia maboresho ya hali ya maisha ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baa la njaa ni janga linaloendelea kutesa mamillioni ya watu, kiasi cha kushindwa kuchangia katika mchakato wa maendeleo endelevu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendelea kubainisha mikakati itakayoiwezesha Jamii kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa watu wengi zaidi; kwa kuzingatia matumizi safi na lishe bora kwa watu wengi. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na maboresho ya huduma ya afya. Bei ya mazao ya chakula inapaswa kusimamiwa kikamilifu ili wajanja wachache wasipate mwanya wa kujitajirisha kwa kupandisha bei kwa ajili ya mafao ya binafsi.

Wajumbe wamegusia kwa kina na mapana tatizo la wahamiaji na vyanzo vyake; dhamana na mchango wa familia katika kudhibiti tatizo la mfumuko wa wahamiaji kimataifa na jinsi ya kuwashirikisha wahamiaji kwa kuzingatia: kiwango cha elimu, lugha na tamaduni za watu husika.







All the contents on this site are copyrighted ©.