2013-11-06 14:57:12

Wakristo wanaalikwa kujenga ushirika kamili na Kristo kwa njia ya Sakramenti, karama na mapendo ili kuishi wito wao vyema!


Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake iliyopita, alitafakari kuhusu ushirika wa watakatifu, kama kielelezo cha mshikamano na watakatifu. Akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro uliokuwa umefurika na umati wa watu, Jumatano tarehe 6 Novemba 2013 amegusia ushirika katika mambo ya kiroho yaani: ushirika katika imani, ushirika wa Sakramenti, ushirika wa karama pamoja na ushirika wa mapendo kama unavyofafanuliwa na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.

Baba Mtakatifu anasema, ushirika wa Sakramenti ni kielelezo makini cha mshikamano miongoni mwa waamini kinachowasaidia kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia na kwa njia yake, wanawezeshwa kukutana na ndugu zao katika imani. Kwa njia ya Sakramenti za Kanisa yaani Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu mwamini anashirikishwa kwa Kristo pamoja na Jumuiya ya waamini, kwani Kanisa linatengeneza Sakramenti na Sakramenti zinaliunda Kanisa na hivyo kuwaunda Watu wa Mungu kwa kuimarisha utambulisho wao.

Kila wakati waamini wanapokutana na Yesu kwa njia ya Sakramenti Yeye mwenyewe anawakirimia wokovu na kuwatuma kuwashirikisha wengine wokovu huo ambao wamebahatika kuuona, kuugusa, kukutana nao na kuupokea kwani hiki ni kielelezo cha upendo. Sakramenti zinawahamasisha waamini kuwa ni Wamissionari wanaotumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu katika medani mbali mbali za maisha, ili kuwashirikisha watu mpango wa ukombozi kutoka kwa Mwenyezi Mungu anaopania kuwashirikisha wote. Sakramenti zinawaimarisha waamini katika imani na furaha ili kuweza kuyashangaa matendo makuu ya Mungu pamoja na kusimama kidete kupinga miungu ya dunia hii.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, ushirika wa karama ni zawadi ya Roho ya Mtakatifu katika maisha ya kiroho kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa na mafao ya Watu wa Mungu, mwaliko na changamoto ya kuishi kwa uaminifu karama hizi za Roho Mtakatifu kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya husika. Karama hizi ni muhimu sana katika mchakato wa utakatifu na utume wa Kanisa. Kila mwamini anaalikwa kuheshimu karama zake na zile za wengine kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, ushirika wa mapendo ni muhimu sana katika maisha ya Jumuiya ya Kikristo na kwamba, ni njia ya kukua katika upendo, kwa kushiriki katika furaha, mateso na mahangaiko ya wengine pamoja na kuthubutu kusaidia kubebea mizigo ya maisha ya maskini na wanyonge ndani ya Jamii. Mshikamano huu ni kiini cha cha umoja miongoni mwa Wakristo. Ni sakramenti na kielelezo cha upendo wa Mungu kwa ajili ya wote kwa kuguswa na furaha na mahangaiko ya jirani.

Baba Mtakatifu anasema, kwa bahati mbaya, waamini wanajikuta wakiwa baridi pamoja na kutoguswa na mahangaiko ya wengine badala ya kuwashirikisha upendo wa kidugu, wanatema cheche za machungu na masikitiko, ubaridi na ubinafsi. Baba Mtakatifu anawaambia waamini na watu wenye mapenzi mema kwamba, Yesu anawaalika kujenga ushirika kamili pamoja naye kwa njia ya Sakramenti, Karama na Mapendo, ili kuishi mintarafu wito wa maisha ya Kikristo.

Baba Mtakatifu alipata fursa ya kuzungumza na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao tangu alfajiri na mapema walianza kujaza pole pole Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ametumia fursa hii kuwashukuru wote kwa matendo makuu yanayojionesha kwa njia ya uwepo wao mjini Vatican. Amewapongeza Mapadre kutoka Uingereza wanaofanya Jubilee ya maisha na wito wa Kipadre. Anawaalika waamini kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwakumbusha waamini kwamba, Mwezi Novemba, Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaombea waamini marehemu ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu. Waamini wanahimizwa kutembelea na kusafisha makaburi.

Msalaba wa Kristo ni alama na kielelezo cha upendo, huruma, upatanisho na matumaini. Anawataka waamini kuendelea kujichotea matumaini na nguvu wanayohitaji katika utekelezaji wa dhamana yao ya kitume miongoni mwa ndugu zao katika Kristo. Amewatakia wote baraka zake za kitume!







All the contents on this site are copyrighted ©.