Mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, 5-19 Oktoba
2014
Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayofanyika
kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014 kwa kuongozwa na kauli mbiu "changamoto
za kichungaji ndani ya familia mintarafu mchakato wa Uinjilishaji", yameanza na tayari
hati ya maandalizi ya Sinodi hii imewasilishwa kwa wadau mbali mbali ili waanze kuifanyia
kazi na kutuma mchango wao kwenye Sekretarieti ya Sinodi mwishoni mwa Mwezi Januari,
2014.
Hayo yamebainishwa na viongozi wakuu wa Sinodi maalum ya Maaskofu kwa
ajili ya Familia wakati walipokuwa wanazindua rasmi hati ya kufanyia kazi. Askofu
mkuu Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia
anasema kwamba, Sinodi hii inapenda kutafsiri kwa namna ya pekee, mawazo na nia za
Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto za kichungaji
mintarafu maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.
Maadhimisho
ya Sinodi hii yatafanyika katika awamu kuu mbili: Awamu ya Kwanza ni kwa ajili ya
kusikiliza shuhuda kutoka kwa Maaskofu katika mchakato wa kutangaza na kuishi kwa
uaminifu Injili ya Familia. Awamu ya Pili ya Maadhimisho ya Sinodi hii yatafanyika
mwaka 2015 kwa kutoa fursa kwa Mababa wa Sinodi kuibua mbinu mkakati wa kichungaji
kuhusu binadamu na familia. Wadau na wahusika wakuu katika Maadhimisho ya Sinodi hii
wamekwishapelekewa Hati ya Maandalizi ya Sinodi.
Lengo la Baba Mtakatifu Francisko
ni kuhakikisha kwamba, Maaskofu wanajenga na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni
mwao katika kukabiliana na changamoto za kichungaji, changamoto iliyotolewa na Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, mawazo ambayo kwa sasa yanapaswa kumwilishwa katika
maisha na utume wa Kanisa.
Pili, Baba Mtakatifu anapenda kuimarisha dhamana
na kazi ya Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu inayofanya kazi bega kwa bega na Khalifa
wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa majukumu yake. Haya ni kati ya mabadiliko
makubwa anayopania Baba Mtakatifu kwa sasa kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa
la Kiulimwengu.
Askofu mkuu Baldisseri anasema, mmong'onyoko wa tunu msingi
za maadili, maisha ya kiroho na utu wema katika ulimwengu mamboleo ni mambo yanayohitaji
mikakati makini ya shughuli za kichungaji. Sinodi hii itawahusisha viongozi mbali
mbali wa Kanisa. Hati ya Maandalizi ya Sinodi ina utangulizi wa jumla, Mafundisho
ya Biblia kuhusu Familia, Mafundisho ya Viongozi wa Kanisa pamoja na maswali dodoso
yanayopaswa kuangaliwa na kujibiwa kwa ukamilifu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
sehemu mbali mbali za dunia.
Majibu ya Maaskofu yatatumwa kwa Sekretarieti
ya Sinodi mwishoni mwa Mwezi Januari, 2014 na kufanyiwa kazi na Sekretarieti ya Sinodi
mwezi Februari, ili kutengeneza "Hati ya Kutendea Kazi" Yaani, Instrumentum
Laboris kwa ajili ya Mababa wa Sinodi.
Kardinali Peter Erdo, Mwezeshaji
mkuu wa Maadhimisho ya Sinodi ya tatu ya Maaskofu kwa ajili ya Familia amegusia kwa
muhtasari yale yaliyojiri kwenye Hati ya ya Maandalizi kwa ajili ya Maadhimisho ya
Sinodi na kwamba, inajikita zaidi katika mambo msingi ya Sheria za Kanisa na mwelekeo
wa shughuli za kichungaji mintarafu maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na
Jamii katika ujumla wake. Sehemu ya pili ya hati hii inazungumzia Kanisa na Injili
ya Familia kwa kujikita zaidi na zaidi kwenye Maandiko Matakatifu, taalimungu, maisha
ya kijamii na kisheria. Sehemu ya tatu ni maswali dodoso yanayogusa maswala nyeti
na tata katika maisha na utume wa Familia nyakati hizi.
Mama Kanisa anapenda
kuipembua dhana ya Familia mintarafu maisha ya ndoa, kwa kutambua kwamba, Familia
ipo kwa sababu imenuiwa na Mwenyezi Mungu mintarafu sheria maumbile, uhuru wa mtu
unaoongozwa na dhamiri nyofu ambayo kimsingi ni sheria ya Mungu katika undani wa mwanadamu.
Kumbe, Ndoa na Familia ni sawa na chanda na pete anasema Kardinali Erdo. Hii inatokana
na ukweli kwamba, mwanaume na mwanamke wanakamilishana katika mapendo kamili, wakiwa
tayari kupokea zawadi ya watoto kutoka kwa Mungu. Ndiyo maana Maaskofu wanaulizwa
kuhusu sheria za nchi zao kuhusiana na masuala ya ndoa.
Maswali dodoso yanawachangamotisha
waamini kutoa maoni yao kuhusu sheria maumbile ya uhusiano kati ya bwana na bibi,
ili kuweza kupata majibu muafaka kuhusu ndoa zinazofungwa Kiserikali kwa kutambua
umuhimu wa familia katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii kwa ujumla kama walivyofafanua
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa linapenda kuangalia pia changamoto
zinazoendelea kujitokeza katika familia hasa kutokana na ubinafsi na uhuru usiokuwa
na mipaka, kiasi hata cha kwenda kinyume na maumbile pamoja na mpango wa Mungu katika
maisha ya mwanadamu.
Wanandoa wanapaswa kuwa waaminifu kwa mpango wa Mungu
katika maisha ya ndoa na familia, kwa kujitahidi kufahamu Mafundisho ya Kanisa kuhusu
ndoa na familia, kama yalivyofafanuliwa na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Sheria
za Kanisa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Wanandoa watambue umuhimu wa Sakramenti
ya Ndoa na masharti yake, kwa kuonesha dhamiri nyofu.
Ndoa miongoni mwa wabatizwa
ni Sakramenti ya umoja na mapendo yasiyogawanyika. Ndiyo maana kwenye maswali dodoso,
Maaskofu wanaulizwa kuhusu maandalizi ya wanandoa watarajiwa katika Majimbo na Parokia
zao na jinsi ambavyo wanandoa wanaweza kusaidiwa na Parokia pamoja na vyama vyao vya
kitume! Ndoa za watu wa jinsia moja zinazungumziwa pia katika maswali dodoso, kwani
hili ni kati ya maswali na hali tete inayozikabilia familia nyingi katika nchi zinazoendelea.
Hali hii inahitaji kufanyiwa tafakari ya kina ili kuibua majibu muafaka katika maisha
na utume wa Ndoa na Familia.
Wanandoa walioachika na kuamua kuoa au kuolewa
tena ni kati ya changamoto za shughuli za kichungaji kwa wakristo wengi, kwani kati
yao kuna wale wanaodhani kwamba, wanatengwa na Kanisa kutokana na kutoshirikishwa
maisha ya Kisakramenti hasa Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu, kiini cha
maisha ya ndoa katika mchakato unaopania utakatifu wa maisha! Maswali dodoso yanaangalia
pia jinsi ambavyo mchakato wa kubatilisha ndoa unavyoweza kuharakishwa; elimu na malezi
ya watoto ndani ya familia na umuhimu wa Mapadre kuwa waaminifu kwa masharti ya maungano
kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa.
Kardinali Peter Erdo anasema kwamba,
Jamii inapaswa kutambua kwamba, Familia ni zawadi ya pekee kabisa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu inayopaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa, ili iweze kutekeleza wajibu na
dhamana yake ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.
Askofu mkuu Bruno
Forte, Katibu mkuu maalum wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia anasema, Baba
Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia kwa namna ya pekee, umoja na mshikamano miongoni
mwa Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika maisha na utume wa
Kanisa mintarafu Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Anataka
kujenga na kuimarisha utamaduni wa Mama Kanisa kusikiliza kwa makini kilio cha watoto
wake ili kukabiliana kwa ujasiri mkubwa na changamoto zinazojitokeza katika maisha
na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla, daima kwa kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa mafao, ustawi, maendeleo ya familia, utu na heshima ya binadamu. Huu
ni mwaliko wa kufanya hija na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha
na utume wa Kanisa.
Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia inatoa kipaumbele
cha kwanza katika mchakato wa Uinjilishaji kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti
ya Wokovu inayotumwa kutangaza Injili ya Kristo kwa watu wote. Baba Mtakatifu anawaalika
Maaskofu kuangalia umuhimu wa familia na changamoto zake katika ulimwengu wa utandawazi,
ili kuokoa roho za watu na kulijenga Kanisa; kwa kutangaza kwa ari na mwamko mpya
Injili ya Familia. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kukabiliana na changamoto za mmong'onyoko
wa tunu msingi za maisha adili na utu wema.
Mama Kanisa anapaswa kusikiliza
kwa makini matatizo na matumaini ya familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia; ili
familia iweze kupendwa na kuthaminiwa tena; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa zawadi
ya maisha, utu na heshima ya binadamu. Familia ni shule ya ubinadamu uliotajirishwa,
mwaliko kwa waamini kujitaabisha kuyafahamu Mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia
ili kugundua utashi wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Yesu Kristo.
Ukarimu
na huruma ni mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anayapatia kipaumbele cha pekee
katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni tunu wanazopaswa kumegewa
wale ambao wana madonda ya maisha ya ndoa na familia. Injili ya Familia inapaswa kuhubiriwa
kwa wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili waonje huruma na upendo wa Mungu
unaokoa na kuponya!
Askofu mkuu Bruno Forte anakiri kwamba, changamoto za maisha
na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo ni nyingi na ni tete kabisa! Ndoa za
watu wa jinsia moja; haki ya malezi kwa watoto; maana ya familia na ndoa yenyewe!
Udumifu na uaminifu wa wanandoa; Myumbo wa maisha ya kiimani kwa wanandoa walioachana
na kuamua kuoa au kuolewa tena.
Zote hizi ni changamoto za kichungaji kwa
sasa. Mama Kanisa anawaalika watoto wake wote kwa unyenyekevu na moyo mkuu kusindikiza
mchakato wa maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia
kwa njia ya Sala na Sadaka yao, ili Roho Mtakatifu aweze kuwaangazia waamini yale
yanayofaa kwa ajili ya kutoa ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Hati
hii ya Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia imehaririwa na Padre
Richard A. Mjigwa. C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.