Kuelekea Bagamoyo! Simameni kidete kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo!
Msikatishwe tamaa!
Askofu mkuu Paul Ruzoka, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania katika mahojiano na Radio Vatican anasema, Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani nchini Tanzania yamekumbana na changamoto na kinzani za kidini hasa Zanzibar
ambako kimsingi ni Mlango wa Imani kwa Waamini wa Kanisa Katoliki Afrika Mashariki.
Uvunjifu wa
misingi ya haki, amani na utulivu ni dosari kwa watu wote wenye mapenzi mema na kwamba,
vitendo hivi vimesababisha hofu na mashaka kwa Wakristo Visiwani Zanzibar na Tanzania
kwa ujumla kwani vitendo hivi vinagusa haki msingi juu ya uhuru wa kidini. Vitendo
hivi vinapaswa kudhibitiwa na vyombo vinavyohusika na wahalifu wapelekwe mbele ya
sheria, ili sheria iweze kushika mkondo wake. Wananchi wajenge utamaduni wa kuheshimiana,
kuthaminiana na kusaidiana kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kudumisha amani,
utulivu, upendo na mshikamano wa kidugu.
Askofu mkuu Ruzoka anasema, pamoja
na changamoto zote hizi, Wakristo wanapaswa kumakubali, kumpokea na kumshuhudia Kristo
aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa maneno na matendo yao adili. Damu ya Wakristo inayomwagika
Visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni kielelezo cha ukomavu wa imani na itazaa
matunda kwa wakati wake.
Askofu mkuu Ruzoka anasema, wavunja sheria, amani
na utulivu miongoni mwa jamii wasionewe soni! Wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria
ili amani na utulivu viweze kurejea tena. Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kwamba,
inasimamia kwa ukamilifu haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anahitaji amani
na utulivu katika kutekeleza mikakati ya maisha. Kumbe, wenye dhamana hii wasifanye
mchezo, Tanzania inaweza kujikuta inatumbukia kwenye "majanga".