2013-11-06 07:22:38

Bila maisha, haki nyingine zote za watoto hazina maana!


Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anapongeza taarifa ya Umoja wa Mataifa kuhusu harakati za kuenzi, kulinda na kutetea haki za watoto zinazokwenda sanjari na mchakato mzima wa kutetea maisha ya watoto, ustawi na maendeleo yao. Anasema, bila maisha, haki nyingine zote za watoto hazina maana yoyote! RealAudioMP3

Inafurahisha kusikia kwamba, magonjwa yanayosababisha vifo vya watoto wadogo yanaweza kwa kiasi kikubwa kudhibitiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Juhudi hizi hazina budi kuhakikisha kwamba, hata haki ya watoto ambao bado hawajazaliwa inalindwa na kuheshimiwa. Hii ni haki ambayo mtoto kabla, wakati na baada ya kuzaliwa anapaswa kupewa bila ubaguzi wa aina yoyote ile! Watoto wasibaguliwe kutokana na ulemavu wao tangu wakiwa bado tumboni mwa mama zao, kwani hata hawa ni watoto wenye haki na heshima yao kwa jamii.

Askofu mkuu Chullikati akitoa hoja kwenye kikao cha kamati ya 68 Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lililokuwa linafanya mkutano wake mjini New York hivi karibuni, alisema kwamba, ujumbe wa Vatican haukubaliani na dhana inayodhalilisha watoto wenye ulemavu kana kwamba, wao si binadamu. Maboresho ya afya kwa watoto hayana budi kuzingatia ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na mchakato wa Umoja wa Mataifa utakaoziwezesha familia kutekeleza wajibu wake wa malezi na makuzi kwa watoto wao.

Watoto wawezeshwe kisheria kupata malezi na makuzi yanayomgusa mtu mzima: kimwili, kiakili, kimaadili, kiroho na kijamii mintarafu: uhuru, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili wasitumbukizwe kwenye biashara haramu ya binadamu pamoja na biashara ya ngono inayonyanyasa utu na heshima ya watoto hawa. Familia hazina budi kuwa ni mahali pa kwanza ambamo watoto wanapata ulinzi na malezi makini. Wazazi wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba, wanawapatia watoto wao mahitaji msingi kwa ajili ya maisha, makuzi na maendeleo yao.

Askofu mkuu Chullikatt anaendelea kusema kwamba, Serikali pia zinawajibu wa kuhakikisha kwamba, familia zinalindwa na kuwezeshwa kikamilifu ili ziweze kutekeleza wajibu na dhamana yake. Familia nyingi kwa sasa zinaendelea kuathirika kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa, umaskini, magonjwa, ukosefu wa fursa za ajira na huduma msingi za maisha ya kijamii.

Matokeo yake, wazazi wengi wanajikuta wanashindwa kutekeleza wajibu na dhamana kwa watoto wao, hali ambayo inagumisha maisha ya watoto ndani ya familia. Familia zinapaswa kuwa ni mahali ya amani, haki, upendo na mshikamano. Magomvi na kinzani ndani ya familia yanaathari kubwa katika malezi na makuzi ya watoto.

Matumizi haramu ya dawa za kulevya, ukorofi wa baadhi ya watoto ni matokeo ya magomvi ndani ya familia. Kumbe, watoto wanahitaji kupata mazingira bora yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika majiundo endelevu na kwamba, familia iwe ni mahali pa kwanza kabisa pa uhakika na usalama wa makuzi na maendeleo ya watoto ndani ya Jamii.

Haki za watoto zinaweza kulindwa ikiwa kama haki msingi na tunu bora za maisha ya kifamilia zitalindwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa na wengi. Uhuru wa kidini, malezi kuhusu masuala ya uzazi, ndoa na familia pamoja na tunu msingi za familia ni mambo ambayo wazazi wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ili waweze kuwarithisha watoto wao bila kuingiliwa! Hii inatokana na ukweli kwamba, kwa njia hii, wazazi wanaweza kuwajibika zaidi kwa watoto wao!

Askofu mkuu Chullikatt anasema kwamba, kimsingi ujumbe wa Vatican haukubaliani kamwe na elimu inayotolewa kwa watoto kuhusu uzazi salama, jambo linalowatumbukiza watoto hao kwenye dhana ya “utoaji salama wa mimba”, vitendo vinavyoendeshwa na Serikali. Hakuna utoaji mimba wowote ambao ni salama, kwani haya ni mauaji na ni vitendo vinavyoacha madhara makubwa kwa wanawake.

Ujumbe wa Vatican unapenda kukazia utamaduni wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba. Watoto wana haki ya kulindwa: kabla, wakati na baada ya kuzaliwa. Haki msingi za watoto zilindwe na kuheshimiwa na kwamba wazazi watekeleze wajibu wao kwa kuongozwa na dhamiri nyofu, sheria ya Mungu katika moyo wa mwanadamu. Utoaji mimba usiwe ni kisingizio cha mpango wa kudhibiti uzazi.








All the contents on this site are copyrighted ©.