2013-11-05 14:56:18

Ubalozi wa Vatican nchini Syria washambuliwa kwa bomu!


Askofu mkuu Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Syria anasema kwamba, ubalozi wa Vatican nchini humo, siku ya Jumanne tarehe 5 Novemba 2013 umepigwa kombora, lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa na shambulio hili, mawazo yake kwa wakati huu anayaelekeza hasa kwa watoto, wanawake na wazee wanaoendelea kuteseka kutokana na kinzani na mgogoro wa kivita nchini Syria.

Askofu mkuu Zenari anasema, bomu hili limerushwa wakati wa asubuhi, muda ambao mara nyingi wanakua Kanisani kwa sala ya asubuhi na Ibada ya Misa Takatifu. Hakuna madhara makubwa, isipokuwa watu wamepata wasi wasi mkubwa ingawa si mara ya kwanza ubalozi wa Vatican nchini Syria kutikiswa na majanga kama haya!

Mashambulizi haya yanaendelea pia kuharibu majengo na mali ya Kanisa kama ilivyotokea hivi karibuni kwenye Konventi ya Wafranciskani mjini Alepo na kwamba, kwa hakika vita haina macho na maisha ya kila mtu nchini Syria yako hatarini. Hakuna anayefahamu kwa sasa sababu ya mashambulizi dhidi ya maeneo ya Kanisa. Mwanzoni, maeneo haya yalikuwa yanaheshimiwa, lakini kwa sasa usalama uko mashakani si tu kwa upande wa Kanisa peke yake, bali kwa wananchi wote wa Syria.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Zenari kwamba, juhudi za kidiplomasia zinazofanyiwa kazi kwa sasa kwa ajili ya mkutano wa amani nchini Syria huko Geneva, utaweza kuzaa matunda ya amani na utulivu, ingawa bado wapinzani wamegawanyika. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, amani na utulivu vinapatikana nchini Syria kwani watu wengi wanaendelea kuteseka kutokana na mgogoro wa kivita.







All the contents on this site are copyrighted ©.