2013-11-05 10:21:23

Sanaa ndani ya Kanisa inajukumu na wajibu wa Kuinjilisha!


Baba Mtakatifu Francisko anasema sanaa, muziki, picha pamoja na utamaduni wa kuhifadhi mambo ya kale ni mambo muhimu katika mchakato wa ukombozi wa ulimwengu. Kwa maneno machache ni kwamba, uzuri unawaunganisha waamini ili hatimaye, waweze kukua na kukomaa katika safari ya imani inayoadhimishwa; matumaini ya Kinabii na upendo unaomwilishwa kama kielelezo makini cha imani tendaji katika maisha ya mwamini.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Wanakwaya wa Sinodi ya Upatriaki wa Moscow ambao wako mjini Roma kwa ziara ya kiekumene. Jumapili iliyopita, majira ya jioni, Kwaya hii imetumbuiza kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma na kwamba, Jumapili ijayo, Wanakwaya watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, mjini Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu umesomwa kwa niaba yake na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Anasema, licha ya tofauti mbali mbali zilizojitokeza katika historia ya Makanisa haya mawili, lakini bado yameendelea kuunganishwa pamoja kwa njia ya Sanaa inayomwezesha mwamini kufanya tafakari ya kina kuhusu ujumbe unaofumbatwa katika sanaa hii.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kubainisha kwamba, sanaa ndani ya Kanisa linalenga kwa namna ya pekee kukoleza mchakato wa Uinjilishaji, changamoto kwa waamini wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi kuendeleza juhudi za majadiliano ya pamoja, ili kuhakikisha kwamba, umoja kamili unapatikana kama Yesu alivyowaombea wafuasi kwa Baba yake wa mbinguni. Sanaa za Kikristo bado zinaweza kuwaunganisha waamini katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu.

Jumapili iliyopita, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na Kwaya hii kwa kitambo kifupi, kwenye makazi yake ya muda kwenye Hostel ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.