2013-11-05 08:43:53

Nimeishi na Mtakatifu kwa kipindi cha Miaka 40, maajabu ya Mungu!


Maisha ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili yalisheheni ushupavu wa Kiinjili uliojionesha tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, akitoa mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kumfungulia Kristo malango ya maisha yao pasi na woga wala makunyanzi.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili amekumbana na majanga katika hija ya maisha yake hapa duniani, mpaka dakika ile ya mwisho bila hata ya kujikatia wala kukatishwa tamaa. Imepita miaka tisa tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipofariki dunia, utadhani ni siku chache tu zilizopita! Ni maneno ya Kardinali Stanslaw Dziwisz wakati wa uzinguzi wa kitabu chake alichoandika kuhusu hija ya maisha yake na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili ambaye anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu hapo Mwakani.

Kitabu hiki ambacho kimeandikwa kwa lugha ya Kitalia kinajulikana kwa jina la "Ho visuto con un santo", kina kurasa 220 zilizopambwa kwa picha za kumbu kumbu ya maisha ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili. Anasema, katika hija ya mahangaiko yake ya ndani, alifarijika kwa sala na alijitahidi kuyaweka yote mikononi mwa mapenzi ya Mungu, ingawa halikuwa ni jambo rahisi, hasa wakati ule Baba Mtakatifu alipokuwa anaendelea kudhoofu zaidi na zaidi. Kardinali Stanslaw anasema, hapo alikubali mpango wa Mungu na kuanza kupata matumaini mapya katika maisha yake.

Anasema, haikuwa rahisi kufuta kumbu kumbu ya maisha ya miaka 40 bega kwa bega na Yohane Paulo wa Pili. Wakati wote huu, wamesali, wamekula na kutaabikiana kwa pamoja, kama ilivyojitokeza mwaka 1981 alipolazimika kumbeba Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili mikononi mwake, alipokuwa amepigwa risasi pale kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, matukio kama haya si rahisi kufutika katika maisha ya mtu! Wakati wa hija za kichungaji, daima alikuwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, akabahatika kutembeleana nchi nyingi duniani na kufahamiana na watu kutoka mataifa, makabila, lugha na jamaa.

Amekuwa ni mfano na kielelezo makini katika maisha na huduma ya Kanisa la Ulimwengu. Tangu alipofariki dunia, kuna umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema wanaomiminika kila siku kwenye Kaburi la Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kwa ajili ya kusali, wakimshukuru Mungu na kuomba rehema na huruma yake. Hii inaonesha kwamba, kwa watu wengi, Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili bado yuko hai katika hija ya maisha yao ya kiroho.

Kumbe, kitabu hiki kinalenga kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwona tena na tena Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili katika hija ya maisha yao! Maisha yao ya pamoja kwa kipindi cha miaka 40 yamemletea mabadiliko makubwa na ukomavu wa imani, matumaini na mapendo. Umati mkubwa wa waamini uliofurika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na viunga vyake, wakati wa mazishi kilikuwa ni kielelezo cha imani, kwani watu wengi walimwona jinsi alivyopambana na majanga ya maisha kwa imani, akajiandaa kukabiliana na fumbo la kifo kwa saburi na moyo mkuu.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alijitosa kimasomaso kwa ajili ya: Kristo na Kanisa lake, akatamani kuona Injili inatangazwa hadi miisho ya dunia kwa njia ya ushuhuda wa maisha; mwanadamu akipewa kipaumbele cha pekee katika kukabiliana na changamoto za maisha. Mungu na mwanadamu ni mambo ambayo yalikuwa na nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II. Kwa hakika ameacha sehemu ya urithi wake kwa mamillioni ya watu duniani.

Kwa upande wake, Kardinali Camillo Ruini, aliyekuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma kwa kipindi cha miaka mingi anasema, kitabu cha kwanza kilichoandikwa kuhusu maisha ya Papa Yohane Paulo II, kilichochapishwa kunako Mwaka 2007, kilimwezesha kwa kiasi kikubwa kumfahamu Yohane Paulo II, maisha, wito na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, licha ya ukweli kwamba, kwa kiasi kikubwa walikuwa karibu katika utume na maisha ya Kanisa Jimbo kuu la Roma.

Kardinali Ruini anaiangalia mikakati ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kwa ajili ya Kanisa, kwa kutaka kuleta mabadiliko ya ndani, kwa kujenga na kuimarisha uhusiano na Mwenyezi Mungu. Alikazia umuhimu wa kuendeleza urithi wa Imani kwa kukazia Mafundisho tanzu ya Kanisa; mwono mpya wa Kanisa pamoja na kuimarisha mikakati ya shughuli za kichungaji zinazopania Uinjilishaji Mpya unaogusa mahitaji ya mtu: kiroho na kimwili mintarafu Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Mwelekeo huu wa kichungaji unakazia pia umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga dunia inayosimikwa katika misingi ya hakii, amani, upendo na mshikamano wa kidugu; daima wakitegemea kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Aliwachochea waamini kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya majadiliano ya kitamaduni, ili kutoa mwanya kwa tunu msingi za Kiinjili kuweza kuleta mabadiliko ya dhati. Umoja miongoni mwa wafuasi wa Kristo ni jambo ambalo alilipatia msukumo wa pekee.

Kardinali Ruini anasema, Papa Yohane Paulo II amekumbana na majanga, akasimama kidete kulinda na kuitetea imani yake kwa Kristo na Kanisa lake; leo hii ni kielelezo makini cha ushuhuda wa matumaini yasiyodanganya. Ni mtu aliyekazia huruma, msamaha na upatanaisho, bila kusahau umuhimu wa uhuru wa kidini kama msingi wa haki zote za binadamu. Mwenyeheri Yohane Paulo II aliwaalika waamini kujitakatifuza na kujipatanisha na Kristo katika Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.

Mapapa waliofuatia mara tu baada ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wamekabiliaana na changamoto nyingi katika kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, wakati mwingine wamelazimika kubeba uzito wa dhamana hii nyeti mabegani mwao! Haikuwa rahisi pale mwanzoni, Papa Wojtyla kukubaliwa mjini Vatican, pengine Kanisa lilikuwa bado halijawa tayari kuona Khalifa wa Mtakatifu Petro akitoka nje ya Italia.

Lakini, akajitahidi kadiri ya uwezo na maongozi ya Mungu kuhakikisha kwamba, umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia kupitia kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki unajengeka na kuimarika kwa kuongozwa na kanuni ya auni!

Mwenyeheri Yohane Paulo II alianzisha mchakato wa mabadiliko katika Mabaraza ya Kipapa kwa kukazia umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu mahalia na Khalifa wa Mtakatifu Petro, dhana inayofanyiwa kazi kwa sasa na Baba Mtakatifu Francisko. Papa Yohane Paulo wa II ameonja magumu na madhulumu ya Kanisa katika Karne ya 20; akawaongoza watu wa Mungu kwa imani, matumaini na mapendo makubwa.

Alitamani kuona vijana wanakua na kukomaa katika imani kwa Kristo na Kanisa lake, ndiyo maana akaanzisha Siku ya Vijana Duniani. Aliwataka vijana kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa vijana wengi, Yohane Paulo II ni mfano wa kuigwa. Hivi ndivyo Kardinali Camillo Ruini anavyohitimisha mchango wake wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Kardinali Stanislao Dziwisz kuhusiana na hija ya maisha yake ya miaka 40 pembeni mwa Mwenyeheri Yohane Paulo II.







All the contents on this site are copyrighted ©.