Maaskofu Katoliki Tanzania waridhia MWUCE kuanza mchakato wa kuwa ni Chuo Kikuu Kamili!
Hotuba ya mkuu wa chuo kwenye mahafali ya 6 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Mwenge
(Chuo cha Mt. Augustino cha Tanzania), iliyotolewa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa,
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Mhashamu Askofu Isaac Amani –
Askofu Jimbo Katoliki Moshi na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu
– Mwenge, Mheshimiwa Padre Daktari Pius Mgeni – Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt.
Augustino Tanzania, Waheshimiwa Wajumbe wa Bodi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu
– Mwenge, Mheshimiwa Padre Daktari Philbert Vumilia – Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki
cha Elimu – Mwenge, Waheshimiwa Wakuu wa Vyuo na wageni mbali mbali mliopo hapa, Waheshimiwa
Wahadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu – Mwenge, Waheshimiwa Wanachuo mnaohitimu
leo, Waheshimiwa wanachuo mnaobaki, Wafanya kazi wote wa Chuo Kikuu Kishiriki
cha Elimu – Mwenge, Mabibi na Mabwana,
Utangulizi Tumeanza sherehe za
leo kwa ibada ya Misa Takatifu tukimshukuru Mungu kwa fadhila na baraka zake kwa wahitimu
wetu wa mwaka huu. Tunapoingia katika sehemu hii ya pili ya adhimisho la siku ya leo
napenda kuchukua nafasi hii kwanza kabisa kuwakaribisha Mababa Askofu na wageni wote
katika mahafali haya ya leo. Karibuni sana. Katika ghafla hii ya kuwatunukia wahitimu
vyeti vyao kwa pamoja tunakuja kuwapongeza kwa jitihada na uvumilivu wao hata kufikia
katika kilele cha azma yao ya kufuzu katika masomo. Mwanadamu mtu mzima anapopangilia
maisha yake anakuwa na lengo na linapokamilika hana budi kufurahi. Ikiwa lengo ni
kubwa pia mahitaji ya kulifikia au kulitekeleza nayo yanakuwa makubwa na kwa kadiri
hiyo mtu atahitajika kuwa makini katika kuliendelea lengo lenyewe. Katika juhudi za
kufikia malengo changamoto hazikosekani na hata vipingamizi.
Mara nyingi vipingamizi
vya kuendelea vinatokana na wahusika wenyewe kutozingatia mafunzo na matokeo yake
kushindiwa njiani. Leo tunaadhimisha ushindi siyo kushindwa na kwa sababu hiyo ni
siku ya kuwashangilia wahitimu wetu. Chuo cha Mwenge kinaona fahari kuwatunukisha
vyeti wahitimu mia nne sabini na sita ambao kwa mwaka mmoja, miwili au mitatu wamejitahidi
kufuata mafunzo na hivyo kukidhi viwango vya ufaulu vinavyotarajiwa. Chuo cha Mwenge
daima kimewania kutayarisha wataalamu wenye maadili mema, wenye kujituma na walio
na moyo wa kujenga Taifa la Tanzania.
Maadili ni chachu ambayo inapatikana
kwa upungufu sana katika nchi yetu kwa sasa. Kelele nyingi zinazosema “Ufisadi, wizi
wa mali za umma, n.k.” ni dalili tosha za maadili kushuka. Lengo la Chuo chetu ni
kuchochea na kujenga maadili mema yaliyo ndani ya mioyo ya mwanadamu ili mwanadamu
aweze kuishi maisha manyofu na ya kujali jamii kwa ujumla wake na majirani kwa upeke
peke katika maisha ya kila siku. Nchi inashikwa na simanzi kwa sababu ya ubinafsi
ambao unapelekea kupenda mali kuliko kujenga jamii inayojaliana na kupendana.
Tabia
na maisha ya Kiafrika yalifunza na kusisitiza sana maisha ya pamoja na kusaidiana
lakini mwelekeo wa walio wengi leo ni kupata mali kwa haraka na bila kujali yanavyopatikana.
Hali hiyo inaleta fujo katika maisha ya jamii na hadi kupelekea kutoaminiana na mwisho
kupigana ndugu na ndugu na jirani na jirani mwenzake. Hayo ni kati ya mambo ambayo
tunatazamia kwamba wasomi wetu wakiwemo wahitimu wetu wa leo wataenda kuyapiga vita
ili maisha ya Mtanzania yawe ya kujali, kutumikia kwa upendo na kufanya kazi kwa weledi
kulingana na mbinu na taratibu zilizopo.
MWUCE na Elimu Kwa wale wageni
ambao hawaifahamu MWUCE niseme tu kwa ufupi kwamba ilikuwa azma ya Baraza la Maaskofu
katika Kikao chake cha 1994 kwamba Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania kianzishwe
Mwanza na kiwe na vyuo vishiriki vitatu yaani: Bugando kwa ajili ya mafunzo ya udaktari,
MWUCE kwa ajili ya Elimu na Ruaha kwa ajili ya sheria na Kompyuta. Hayo yamefanyika
kwa utaratibu huo na kuongeza vyuo vingine nane hadi sasa. Mwenge tangu awali imejishughulisha
na kutayarisha walimu wa masomo ya Sayansi na inafahamika hivyo. Tunayo pia masomo
ya Sanaa na masomo mengine ambayo yameanzishwa kwani wajibu wa chuo kikuu ni kufundisha
masomo mbali mbali lakini kila chuo kina eneo maalumu kinapojikita.
MWUCE imeendelea
kuimarisha eneo la utayarishaji wa waalimu jambo ambalo ni moja ya mahitaji makubwa
Kitaifa. Nchi inapohangaika na tatizo la ufaulu mdogo wa wanafunzi katika shule za
msingi na sekondari Chuo cha Mwenge kinaguswa sana na jambo hilo kwani mchango wake
kwa jamii hutokana na idadi ya wanachuo wanaohitimu na kwenda kufundisha mashuleni.
Ninatambua kwamba tangu kuwepo kwa Chuo cha Mwenge kimekuwa kinaendesha warsha
za kusaidia walimu wa sekondari kuimarisha taaluma zao za ualimu. Mwaka huu nimesikia
kwamba licha ya kuendesha warsha hiyo chuoni kama ilivyo utaratibu wa kawaida pia
Chuo kikishirikiana na wadau wengine kimeamua kusogeza huduma hiyo karibu na walimu
na wanafunzi na hata kupanua eneo kwenye sekondari 40 katika Wilaya 7 za Mikoa ya
Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Haya yote ni katika jitihada za kuchangia katika kukuza
elimu nchini.
Aidha MWUCE imeendelea kuimarisha Programu yake ya ualimu kwa
kuanzisha shahada ya Uzamili ambapo wanachuo kumi na mmoja watahitimu siku hii ya
leo. Huu ni mchango wa Kanisa katika kuimarisha elimu nchini na hatutasimamia hapo
bali utaratibu ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na Chuo mwaka hadi mwaka
ili tuwe na wataalamu wengi zaidi katika Taifa letu. Jambo ambalo daima jamii inatarajia
kutoka MWUCE na ndicho ninachoamini kinafanyika, ni wakufunzi kuimarisha ufundishaji
ili wahitimu watoke wakiwa wameiva vizuri. Wanafunzi huomba kujiunga na chuo ili kusudi
waje kusoma lakini lengo kuu la mbeleni ni kupata ajira. Ajira ya mhitimu itakuwa
na umaana kwake na kwa jamii kama mwajiriwa huyu atakuwa na nyenzo za kutimiza kazi
yake vizuri. Hapo awali nimezungumzia kuhusu maadili mema lakini mhitimu anahitaji
pia awe amesoma na kuelimika vizuri kuweza kukidhi mahitaji ya ajira. Hivyo ni wajibu
wa wahadhiri na wanachuo kuwania kufanya kazi kwa pamoja kwa nia ya kumtayarisha mtaalamu
mahiri wa baadaye. Kama mwanachuo kazania kile unachokisoma ili uwe mtaalamu hodari.
MWUCE ipo ikuongoze na kukufundisha siyo kwa elimu ya kitabuni peke yake bali pamoja
na mafunzo kwa vitendo.
Mafunzo kwa vitendo kwa upande wa MWUCE yamepewa kipaumbele
sana ili kusudi wanachuo wakiwa mafunzoni waanze kujijengea ujuzi wa kazi wanayoisomea.
Kwa wale wa ualimu najua kwamba wanaenda kufanya ufundishaji “Teaching Practice” –
zoezi hili mahali pengi limechukuliwa kama utaratibu wa kawaida wa kumpatia mwanachuo
alama baada ya ukaguzi wa mazoezi yanayofanywa na wahadhiri wa Chuo. Kwa upande wa
MWUCE zoezi hili ni la muhimu sana na hivyo linapewa uzito maalumu.
Ninajua
kwamba Mwenge imeanzisha utaratibu siyo tu wa wahadhiri kuwatembelea wanachuo kwenye
shule wanakofanyia mazoezi bali pia wamechaguliwa waalimu wa sekondari walio wazoefu
wa kutembea na wanachuo walioko mazoezini wakiwashauri katika hiyo safari yao. Utaratibu
huo unalenga kuwajengea wanachuo uwezo na utaalamu ambao utawasaidia kufundisha kwa
umakini na umahiri waingia kwenye ajira. Tafadhali zingatieni hayo mliyoyapata kusudi
hayo mliyoyasoma yasaidie jamii.
Pia kwa masomo mengine yasiyo ya ualimu mnakuwa
na mazoezi kwenye maeneo mbali mbali ili kujipatia utaalamu na kuimarisha ujuzi. Zingatieni
hayo ili mnapomaliza hayo mliyojifunza yawe nyenzo ya kufanya kwa ufanisi katika ajira
yenu.
Changamoto Uendeshaji wa vyuo vya elimu ya juu unazo changamoto nyingi
na hasa katika kipindi hiki. Baraza linatambua changamoto hizo zikiwemo: Ufaulu
mdogo wa wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita na hivyo kufanya idadi ya wanafunzi
wanakidhi viwango vya kujiunga na vyuo kuwa ndogo Mikopo kwa ajili elimu ya juu
kutopatikana kwa ajili ya wanachuo wa programu zote kunafanya wanafunzi wengine kushindwa
kujiunga na chuo Gharama za uendeshaji wa vyuo vikuu kuwa kubwa Uwepo wa wanachuo
vyuoni wasiotilia mkazo masomo badala yake kufuata maisha ya anasa na starehe na hivyo
kutofaulu vizuri kwenye masomo yao
Hayo ne mengine mengi yamekuwa ni changamoto
kwenye vyuo na pia kwa wanafunzi vyuoni. Yale ambayo Mwenye Chuo ana uwezo nayo ataendelea
kuyashughulikia ikiwa ni pamoja na kuuhimiza uongozi wa MWUCE kuongeza programu za
Certificate na Diploma ili vijana wengi waweze kujiunga na Chuo chetu. Aidha tutaendelea
kuwasiliana na serikali yetu kuhusiana na uwezekano wa mikopo kutolewa kwa wanafunzi
wote wanaopokelewa vyuoni. Kwa upande wa wanachuo napenda kuweka msisitizo kwamba
nia ya Kanisa ni kutayarisha wataalamu walio na maadili mema. Pendeni kuwa na tabia
njema ambazo zitakubalika kwenye jamii.
Maamuzi ya Baraza la Maaskofu kuhusu
MWUCE Chuo cha Mwenge kimeanza kutoa mafunzo ya shahada mwaka 2005/06 hivyo sasa
kiko kwenye mahafali ya sita. Kwa hiyo miaka saba Chuo kimekua hadi kufikia hatua
tunayoiona sasa. Idadi ya wanachuo imeongezeka kutoka wanafunzi 58 (31 shahada na
27 stashahada) mwaka 2005/06 hadi 1,960 mwaka 2012/13. Katika kukua huko pia idadi
ya wahadhiri, majengo na vifaa vya kujifunzia na kufundishia vimeongezeka kulingana
na idadi ya wanachuo. Hayo yote yanaonesha kukua kwa Chuo. Kutokana na maendeleo hayo
na kulingana na kukua kwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (kwa sasa kina vyuo
vishiriki na vituo (Centres) 12) Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limeona ni
muda mwafaka wa Chuo Kiuu Kishiriki cha Mwenge (MWUCE) kianze mchakato wa kuwa Chuo
Kikuu kamili. Tayari Mkuu wa Chuo Padre Philbert Vumilia alishapata barua ya maelekezo
na kwa sababu hiyo nawaalika muombee utaratibu huu ufanikiwe.
Nia ya kuazimia
Chuo hiki kiwe Chuo Kikuu kamili ni kusudi kiendelee kuimarisha yale ambayo tumeshayaona
kuwa na mazuri na ya kuijenga jamii ya Tanzania. Hivyo matarajio ya Baraza ni kwamba
Elimu itaendelea kuimarishwa na wahitimu wa Chuo hiki waende kuwa MWANGA kama kauli
mbiu ya Chuo hiki inavyodai. Baraza la Maaskofu Tanzania liko tayari kusaidia kwa
kila njia kuhakikisha kwamba Chuo chetu kinaendelea kutoa elimu bora ya kuwafaa watanzania.
Nawaasa
tena wahadhiri na wanachuo mnaobaki muendelee kujiimarisha ili Chuo kiweze kufikia
malengo yake ambayo ni kufundisha, kutafiti na kutoa huduma kwa jamii. Daima simamieni
kile kitakachojenga jamii kwa uzalendo na nia njema. Maadili mema pamoja na kuaminiana
kutawale maisha yenu ili kila mnachokifanya kilete maendeleo kwa watu.
Kwa
wahitimu wetu, nawapongeza tena kwa hatua mliyofikia mkijua kwamba hatua moja huvuta
hatua nyingine. Nendeni mkahudumie mkiwa mabalozi wazuri wa MWUCE. Kile mlichokisoma
hapa mkakiishi na kukishirikisha kwa wengine. Nanawatakia wingi wa baraka katika maisha
yenu.
Mwisho, napenda kuwashukuru jumuiya yote ya MWUCE kwa shughuli zote wanazozifanya
kukifanya Chuo chetu kiendelee kukua. Ahsanteni sana. Nawatakieni wingi wa baraka
katika huduma zenu mkijua kwamba Baraza la Maaskofu liko nanyi.
Ahsanteni sana,
Mungu awabariki. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa Mkuu wa Chuo Kikuu
Cha Mt. Augustino Tanzania