Mshikamano wa kidugu na ushuhuda kwa Roho Mtakatifu ni mwelekeo mpya katika maisha
na utume wa Makanisa!
Wajumbe wa mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Jumatatu tarehe
4 Novemba 2013 wamekazia umuhimu wa kuonesha mshikamano wa kidugu katika maisha na
katika utekelezaji wa utume na dhamana ya Kanisa katika Uinjilishaji; kwa kuangalia
kwa pamoja changamoto zinazojitokeza katika Uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo.
Wajumbe
hao kimsingi wamekubaliana na hati ya mkutano iliyoandaliwa na Kamati Utume na Uinjilishaji
ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika kikao chake cha Mwezi Septemba, 2012 kilichofanyika
nchini Ugiriki. Hati hii pamoja na mambo mengine inatoa mwelekeo wa Kibiblia, Sala
na Nyimbo zinazoweza kutumika katika kuhamasisha mchakato wa Uinjilishaji unaofanywa
na nchini wanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.
Wajumbe wanakazia umuhimu
wa kushirikiana kwa pamoja kama ndugu kama kielelezo cha umoja katika Roho Mtakatifu
pamoja na kuhakikisha kwamba, Kanisa linawajali na kuwahudumia wale wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Kimsingi wajumbe wanayataka Makanisa kushikamana kama njia ya
kutolea ushuhuda amini katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.