Madonda matakatifu ya Yesu ni kielelezo cha huruma na tumaini la maisha ya uzima wa
milele!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 4 Novemba 2013 ameadhimisha Ibada ya Misa
Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Makardinali na Maaskofu waliofariki
dunia katika kipindi cha Mwaka 2013, kutoka sehemu mbali mbali za dunia hasa katika
Mwezi Novemba, uliotengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu,
ili waweze kupata tuzo waliloahidiwa watumishi wema na waaminifu.
Mtakatifu
Paulo anawaandikia Warumi akisema, kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala
mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo,
wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyochini, wala kiumbe kinginecho chote
hakitaweza kuwatenga na upendo wa Mungu, ulio katika Kristo Yesu, Bwana wao! Upendo
wa Mungu ndicho kielelezo cha matumaini na imani ya Kikristo.
Hakuna jambo
lolote linaloweza kuwatenga waamini kutoka katika upendo wa Kristo, aliyejitoa bila
ya kujibakiza kwa ajili ya wokovu wa walimwengu, changamoto kwa waamini kumpokea kwa
imani thabiti, ili kuendeleza mapambano ya maisha ya kila siku.
Baba Mtakatifu
katika mahubiri yake anaendelea kusema kwamba, ni dhambi peke yake inayoweza kuharibu
upendo wa Mungu, lakini utimilifu wa upendo wa Mungu kwa waja wake unajionesha kwa
namna ya pekee kwa kukutana na hatimaye kuonana na Muingu uso kwa uso, kwani maisha
adili hapa duniani yanafungua mlango wa matumaini ya maisha baada ya kifo.
Baba
Mtakatifu anasema, waamini ambao wamejitahidi kuishi kikamilifu na kutekeleza wajibu
wao barabara kwa ajili ya Kanisa, hapana shaka kwamba, wako mikononi mwa Mwenyezi
Mungu, anayewapokea na kuwalinda; kielelezo cha heshima na uaminifu. Hili ndilo tuzo
wanalostahili viongozi hawa wa Kanisa waliojitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa
Mungu na jirani zao, sasa wako mikononi mwa Mwenyezi Mungu.
Wote wamehifadhiwa
dhidi ya mauti; ni watu ambao wameyasimika maisha yao katika furaha na mahangaiko;
katika matumaini na magumu ya maisha; huku wakiendelea kuwa waaminifu kwa Injili na
ari ya kuokoa roho za watu, sanjari na kutunza mali ya Kundi walilokabidhiwa kwao
na Mama Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata dhambi za waamini ziko
mikononi mwa huruma ya Mungu inayofumbatwa katika upendo. Madonda matakatifu ya Yesu
ni kielelezo cha huruma na tumaini la maisha ya uzima wa milele. Hili ni tuzo linalotolewa
kwa wale wanaopokea Neno la Mungu, daima wakionesha unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu.
Baba
Mtakatifu amewakumbuka Makardinali na Maaskofu waliojitoa bila ya kujibakiza katika
wito na huduma kwa Kanisa; wakapenda kama Bwana harusi anavyompenda mwanamwali wake.
Baba Mtakatifu amewaweka viongozi wote hawa chini ya maombezi ya Bikira Maria na Mtakatifu
Yosefu, ili waweze kuwasaidia kuona Ufalme wa mwanga na amani, mahali ambapo wenye
haki waliojitahidi kuwa waamifu na mashahidi wa Injili wanapoishi.