2013-11-02 14:33:56

Waconsolata kutinga timu Luanda, Angola, hapo mwakani!


Viongozi wakuu wa Shirika la Wamissionari wa Consolata kutoka sehemu mbali mbali za Afrika, hivi karibuni wamehitimisha mkutano wao uliojadili pamoja na mambo mengine, hali ya uchumi kwa Shirika la Waconsolata Barani Afrika pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo.

Wamissionari hawa wanaendelea kumshukuru Mungu kutokana na ukarimu wake kwa kuwajalia idadi kubwa ya miito inayolifanya Shirika kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa hata kwa siku za usoni.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mheshimiwa Padre Dietrich Pendawazima, Makamu mkuu wa Shirika amewataka Waconsolata kuhakikisha kwamba, wanajitamadunisha kwa kuendelea kusoma alama za nyakati ili kuweza kukabiliana na changamoto za Uinjilishaji mpya Barani Afrika, hasa wakati huu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wakuu wa Shirika kutoka Afrika wamewasilisha hali ya uchumi katika maeneo yao na changamoto wanazoendelea kukabiliana nazo hasa kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa.

Padre Pendwazima, amewataka wakuu wa Shirika kuwa makini na wala kutokatishwa tamaa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa na badala yake, wajiwekee mbinu na mikakati makini ya kujitegemea na kulitegemeza Shirika kwa kutumia kikamilifu rasilimali: vitu na watu waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Anasema, hakuna sababu kwa Wamissionari wa Consolata kupandisha "Presha" kwa sababu ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa, badala yake Wamissionari wawe wajanja kusoma alama za nyakati na hatimaye, kuleta mabadiliko makubwa yanayokusudiwa, kwa kuwekeza zaidi na zaidi Barani Afrika.

Wamissionari Waconsolata kwa sasa wanakamilisha maandalizi makubwa kabla ya kufungua shughuli za kitume na kichungaji nchini Angola, kama sehemu ya utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano mkuu wa Shirika uliofanyika kunako Mwaka 2005 nchini Brazil. Angola ina idadi kubwa ya wananchi, lakini waamini wa Kanisa Katoliki wanaunda asilimia 60% tangu baada ya kuhitimishwa kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, takribani miaka kumi iliyopita. Angola ina kiu ya kusikiliza Neno la Mungu linalojikita katika ukweli, haki, amani, upendo na upatanisho wa kitaifa.

Waconsolata wanatarajia kufungua utume huu mjini Luanda, Angola, hapo mwakani, panapo majaliwa. Msumbiji ilikuwa ni nchi ya kwanza kupokea Wamissionari wa Consolata na hapa kuna idadi kubwa ya miito inayopaswa kupaliliwa na kuendelezwa kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika na Ulimwengu kwa ujumla. Mkutano wa wakuu wa Shirika la Waconsolata hukutana kila mwaka na mara mwisho walikutana Bunju, Jijini Dar es Salaam, Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.